Jacky Vike afunguka jinsi alivyowaogopa waigizaji wenzake alipojiunga na Papa Shirandula

Muhtasari

•Jacky alisema kuwa marehemu Charles Bukeko almaarufu kama Papa Shirandula ndiye aliyemshawishi kujiunga na kipindi hicho kwani alikuwa na imani kubwa juu yake.

•Amefichua kuwa haikuwa rahisi kwake wakati alipojiunga na waigizaji wengine wa kipindi hicho ambao tayari walikuwa wamejizolea umaarufu mkubwa tayari.

•Mwigizaji huyo alifichua kuwa mwigizaji aliyemtishia zaidi ni Jacqueline Nyaminde ambaye aliigiza mke wa Papa Shirandula, Wilbroda.

Jacky Vike na marehemu Papa Shirandula
Jacky Vike na marehemu Papa Shirandula
Image: HISANI

Mwigizaji wa zamani wa Papa Shirandula Jacky Vike almaarufu kama Jacky Vike amefunguka kuhusu mazingira magumu aliyojipata katika wakati alijiunga na kipindi hicho.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, mwigizaji huyo alifichua kuwa alikuwa amesusia  kujiunga na kipindi hicho kwa kuwa hakutaka kuigiza kama kijakazi mwenye lafudhi ya jamii ya Luhya.

Jacky alisema kuwa marehemu Charles Bukeko almaarufu kama Papa Shirandula ndiye aliyemshawishi kujiunga na kipindi hicho kwani alikuwa na imani kubwa juu yake.

"Marehemu Bukeko aliniambia kuwa alihisi nina uwezo wa kuchukua nafasi hiyo, nikasema niende tu. Hapa Awinja akazaliwa. Sijui ningekuwa wapi kama singekubali. Yeye ndiye alinipatia fursa hii na kunijengea jina la Awinja" Jacky alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja amefichua kuwa haikuwa rahisi kwake wakati alipojiunga na waigizaji wengine wa kipindi hicho ambao tayari walikuwa wamejizolea umaarufu mkubwa tayari.

Alisema alijishuku sana na kuhisi kutishiwa na waigizaji wenzake kwa kuwa tayari walikuwa wamebobea kwenye ulingo wa uigizaji.

"Nilitishika, hata nilikuwa nashindwa kuigiza. Nilikuwa naona wako na uzoefu mkubwa na wamekuwa katika tasnia ya uigizaji kwa miaka mingi na ni wanoma. Nilijitilia shaka. Kadri muda ulivyosonga nilendelea nikizoea tukafika mahali tulifika" Alisema.

Mwigizaji huyo alifichua kuwa mwigizaji aliyemtishia zaidi ni Jacqueline Nyaminde ambaye aliigiza mke wa Papa Shirandula, Wilbroda.

Jacky alisema alimuogopa zaidi Nyaminde kwa kuwa mwanzoni alimchukulia kama mtu mkali na mwenye kiburi kikubwa. Hata  hivyo alisema hali hiyo ilibadilika baada yao kuzoeana na kwa sasa wao ni marafiki wakubwa.

"Tulikuwa tunaigiza pamoja, lazima tungezoeana. Sikuwa na chaguo. Tulikuja tukawa zaidi ya wafanyikazi wenza tu, sisi ni madada. Saa hii sisi ni familia, huwa tunatembeleana hata ocha" Alisema.

Alifichua kuwa urafiki wake na Nyaminde umedumu kwa takriban miaka kumi huku akieleza kuwa heshima na kuelewana zimechangia zaidi  katika kudumu kwa uhusiano wao.