Namiliki kamisi 9, wasichana wa Nairobi bado wanavaa kamisi- Mwigizaji Jacky Vike

Muhtasari

•Awinja ameweka wazi kuwa vazi hilo ambalo lilidhaniwa kutupiliwa mbali na wanawake wa hapa nchini  bado linaundwa na kuuzwa sokoni.

•Alifichua kuwa kwa sasa anamiliki zaidi ya kamisi tisa ambazo aghalabu huwa anatumia wakati anaigiza.

Jacky Vicky katika mahojiano na Massawe Japanni
Jacky Vicky katika mahojiano na Massawe Japanni

Mwigizaji mashuhuri Jacky Vike almaarufu kama Awinja Nyamwalo kutokana na kipindi cha Papa Shirandula amekiri kuwa yeye ni mteja sugu wa kamisi.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, Awinja alifichua kuwa kwa sasa anamiliki zaidi ya kamisi tisa ambazo aghalabu huwa anatumia wakati anaigiza.

Mama huyo wa mtoto mmoja aliweka wazi kuwa vazi hilo ambalo lilidhaniwa kutupiliwa mbali na wanawake wa hapa nchini  bado linaundwa na kuuzwa sokoni.

"Niko na kamisi za wiki nzima, hizo ni saba. Nadhani nimeongeza zingine mbili, hizo ni tisa. Niko na zingine kama tatu ambazo nimetupa huko. Bado zinauzwa, ziko kila mahali" Awinja alisema.

Mwigizaji huyo alidai kuwa wanawake wengi ikiwemo wale wa jiji kuu, Nairobi wangali wanavaa vazi hilo kisiri.

Alisema kamisi inavaliwa zaidi vijijini ambako kulingana naye, wanawake huonekana kukiuka sheria wanapotembea bila.

"Watu wanavaa kamisi bado. Hata wasichana warembo hapa Nairobi  wanavaa ndani ya dera. Kamisi zinavaliwa sana. Sio mimi pekee nazinunua. Ocha kama hujavalia kamisi uko uchi" Alisema.

Awinja anajulikana kupendelea kuigiza akiwa amevalia mavazi yanayoonekana kuwa ya kikale kama vile kamisi na rinda refu.