"Wewe nami ni hadi milele!" Bilionea Grand P adhihirisha mapenzi kwa mwanasoshaiti Eudoxie Yao

Muhtasari

•Bilionea huyo amesema ataishi kumpenda mwanadada huyo aliyebarikiwa na makalio makubwa kweli katika siku zote za maisha yake.

•Hivi majuzi Eudoxie Yao alimtaja bilionea huyo kama Ex wake baada ya kumuona akijiburudisha na wanadada wengine ndani ya bwawa la kuogelea.

Image: INSTAGRAM// GRAND P

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Guinea Moussa Sandiana Kaba almaarufu Grand P amethibitisha kuwa bado anampenda mwanasoshalaiti Eudoxie Yao miezi kadhaa baada ya  ripoti kuwa wametengana kuenea.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Grand P amesherehekea mwanasoshalaiti huyo kutoka Ivory Coast na kudhihirisha upendo wake  mkubwa kwake usio na mwisho.

Bilionea huyo amesema ataishi kumpenda mwanadada huyo aliyebarikiwa na makalio makubwa kweli katika siku zote za maisha yake.

"Wewe na mimi ni kwa maisha. Shukran" Grand P alimwandikia Bi Yao.

Haya yanajiri takriban miezi miwili baada ya Grand P kudai kapokonywa kipenzi hicho chake na mwanamuziki Roga Roga kutoka Congo.

Picha za  Yao akijiburudisha na Roga Roga zilienezwa mitandaoni na kumtia  Grand P hofu kubwa kuwa huenda  msanii huyo alikuwa amempokonya jiko lake.

Grand P ambaye ana maumbile ya kipekee alimpatia Roga Roga onyo kali  dhidi ya kuendeleza mahusiano na mkewe.

"Ndugu yangu Roga Roga nakuheshimu sana wewe na watu wote wa Kongo... Lakini  njia unayotaka kufuata si ya kupendeza kwako, usifurahie kuwa karibu na mke wangu la sivyo nitachukua hatua mbaya. Hii ni onyo, Asante!" Grand P aliandika.

Takriban miezi sita iliyopita Bi Yao alikuwa ametangaza kutengana kwake na Grand P ila baadae walionekana pamoja mara kwa mara, hakikisho kuwa walirudiana.

Hivi majuzi hata hivyo, Yao alimtaja bilionea huyo kama Ex wake baada ya kumuona akijiburudisha na wanadada wengine ndani ya bwawa la kuogelea.