"Watu bado wanatupenda," Wema Sepetu azungumza baada ya kushinda tuzo ya ma-ex bora na Diamond

Muhtasari

•Diamond alitoa shukrani kwa Wema kwa kufanikisha hayo huku akiwasihi wapenzi wengine kuhifadhi uhusiano mwema hata baada ya kutengana.

•Mwigizaji huyo alisema huenda waliteuliwa kushinda tuzo hilo kwa kuwa watu wengi walipendezwa na mahusiano yao katika kipindi ambacho walikuwa kwenye mahusiano.

Image: HISANI

Mwigizaji Wema Sepetu amezungumza kwa mara ya kwanza baada yake na aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz kutambuliwa kama wapenzi bora wa zamani.

Takriban wiki mbili zilizopita Diamond alipokea tuzo la 'MaEx bora' (wapenzi bora wa zamani) kwa niaba yake na mlimbwende huyo ambaye walitengana naye miaka minane iliyopita.

Akipokea tuzo hilo, Diamond alitoa shukrani kwa Wema kwa kufanikisha hayo huku akiwasihi wapenzi wengine kuhifadhi uhusiano mwema hata baada ya kutengana.

"Kwanza namshukuru ex mwenzangu. Pia natoa ujumbe kwa ndugu zangu wengine, tunapotengana tukae kwa amani. Nashukuru" Diamond alisema katika tamasha ya Mahaba Ndi Ndi Ndi iliyofanyika Mlimani City mnamo Februari 14.

Wapenzi hao wawili wa zamani walishinda tuzo hilo kwa mujibu wa kura za mashabiki waliohudhuria tamasha hiyo iliyoandaliwa maalum kwa malkia wa Bongo Zuchu.

Akizungumza na Bongo5 katika hafla ya kuzindua ubalozi wake na SuperMate, Wema alidai kuwa hakufahamu kabisa maana ya tuzo hilo.

Mwigizaji huyo alisema huenda waliteuliwa kushinda tuzo hilo kwa kuwa watu wengi walipendezwa na mahusiano yao katika kipindi ambacho walikuwa kwenye mahusiano. Hata hivyo alisema kuwa mahusiano yao na kilichotokea kati yao ni mambo ambayo tayari yalitupwa kwenye kaburi la sahau.

"Chochote kilichotokea kati yangu na yeye kilitendeka na imeisha. Ni historia, ni jambo la kitambo na tunaendelea kuishi. Labda ni wanandoa ambao walipendwa zaidi kipindi tulikuwa kwenye mahusiano. Watu bado wanatupenda" Wema alisema.

Wema na Diamond walitengana mwaka wa 2014 baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa kipindi kirefu.