Mpenzi wa Stivo Simple Boy afunguka kuhusu sababu za kuficha mahusiano yao kwa miaka mitatu

Muhtasari

•Pritty Vishy alifichua kuwa urafiki wake na mwanamuziki huyo ulianza miaka sita iliyopita walipokutana kwa mara ya kwanza.

•Vishy amedai kuwa alihofia kuweka mahusiano yake na Simple Boy wazi kwa kuwa yeye bado ni mwanafunzi mwenye umri mdogo

Pritty Vishy na Stivo Simple Boy
Pritty Vishy na Stivo Simple Boy
Image: HISANI

Mwanadada anayeaminika kuwa mpenzi wa mwanamuziki Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amethibitisha kuwa wamerudiana, wiki chache tu baada ya kutangaza kuwa wametengana.

Akiwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, Pritty Vishy alifichua kuwa urafiki wake na mwanamuziki huyo ulianza miaka sita iliyopita walipokutana kwa mara ya kwanza.

Vishy alisema iliwachukua takriban miaka mitatu ya urafiki wa kawaida  kabla ya kuanza kuchumbiana rasmi mwaka wa 2019.

"Tulipatana hapo mwaka wa 2016-2017. Hapo tukaanza kuwa marafiki. Mwaka wa 2019 vile alianza kuvuma ndio tukaanza kuchumbiana" Vishy alisema.

Licha yao kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu, mahusiano ya Simple Boy na Pritty Vishy yamekuja kufichuka hivi majuzi baada ya mwanadada huyo kupakia video yao kwenye mtandao wa TikTok.

Vishy amedai kuwa alihofia kuweka mahusiano yake na Simple Boy wazi kwa kuwa yeye bado ni mwanafunzi mwenye umri mdogo. Vilevile amedai Simple Boy pamoja na usimamizi wake hawakutaka mahusiano hayo yajulikane.

"Sikutaka nijulikane kwa kuwa Simple Boy hakuwa sawa nayo, pia mimi sikuwa sawa nayo. Wasimamizi wake pia hawakutaka tuwe pamoja. Ningeweka wazi ingekuwa shida kwake na pia kwa wazazi wangu. Wasimamizi wake walisema mimi bado ni mwanafunzi mdogo. Walisema naweza mfunga," Alisema

Mwanadada huyo alisema kuwa alimjua Stivo hata kabla ya umaarufu na jambo kuu analopenda juu yake ni unyenyekevu wake.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa huwa hawaishi pamoja kwa kuwa kila mmoja wao ana mambo ya kibinafsi ya kushughulikia.