"Nahisi vibaya sana!" Mulamwah afunguka jinsi kutenganishwa na bintiye kumemuathiri

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alisema kuwa sio jambo la kujivunia kuona binti yake akilelewa kwa nyumba ya mwanaume mwingine ilhali yeye kama babake yupo hai.

•Alisema anamtamani sana bintiye katika maisha yake na hata amemtengea chumba chake maalum ndani ya nyumba ambayo anajenga kwao Kitale.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah amekiri kuwa haridhiki kuona binti yake wa miezi mitano, Keilah Oyando akilelewa mbali naye. 

Akiwa kwenye mahojiano na Sauti TV, Mulamwah alieleza wasiwasi wake kuhusiana na jinsi binti yake anavyolelewa na mpenzi wake wa zamani mwigizaji Carol Muthoni.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa sio jambo la kujivunia kuona binti yake akilelewa kwa nyumba ya mwanaume mwingine ilhali yeye kama babake yupo hai.

"Nahisi vibaya. Kwanza nikijua mtu ananyonyesha na analewa inakuwa noma. Haihisi sawa hasa kwa kuwa mtoto mhusika akiwa msichana. Huyo msichana atakua kwa nyumba ya wenyewe labda siku moja mamake hatakuwa, itakuwa ni ngori.  Msichana anafaa kuwa mikononi mwa babake. Haihisi vizuri," Mulamwah alisema.

Mulamwah alikiri kuwa hajafanikiwa kumuona binti yake kwa kipindi kirefu huku akifichua kuwa mara ya mwisho kumuona alikuwa na umri wa miezi miwili tu.

Hata hivyo alisema anamtamani sana bintiye katika maisha yake na hata amemtengea chumba  maalum ndani ya nyumba ambayo anajenga kwao Kitale.

"Hii nguvu yote ambayo naweka, nyumba tunajenga huko, yeye ndie tunajengea. Chumba chake kiko hapo, ata kama hatakuwa , itakuwa hapo hadi wakati ambao atafika aingie hapo ndani. Kila kitu ambacho nafanya nafanyia mtoto wangu ambaye yuko na ambao watakuja. Naweza kuhisi vizuri akiwa karibu, kusema kweli angekuwa ananipa motisha kutia bidii zaidi na kunipa mwelekeo mzuri wa maishi. Nahisi vibaya sana lakini natumai huko mbele mambo yatakuwa mazuri," Alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa uhusiano mbaya kati yake na mzazi mwenzake umedhoofisha mpango wa kushirikiana katika malezi.