Carol Muthoni afunguka jinsi kuharibika kwa mimba kulichangia kuvunjika kwa mahusiano yake na Mulamwah

Muhtasari

•Mama huyo wa binti mmoja alifichua kwamba alikumbwa na msongo wa mawazo na kukosa utulivu wa akili baada ya kupoteza ujauzito huo.

•Muthoni alifichua kuwa  kuharibika kwa mimba yake pia kulimletea hamu kubwa ya kupata watoto. 

Carol Muthoni katika studio za Radio Jambo
Carol Muthoni katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwigizaji Caroline Muthoni amekiri alikabiliwa na matatizo chungu nzima baada ya kupoteza ujauzito wake wa kwanza takriban miaka miwili iliyopita.

Akiwa kwenye mahojiano na Dr. Ofweneke, Muthoni alidai kuwa masaibu yalianza kukumba ndoa yake na mchekeshaji Mulamwah baada ya mimba kuharibika

Mama huyo wa binti mmoja alifichua kwamba alikumbwa na msongo wa mawazo na kukosa utulivu wa akili baada ya kupoteza ujauzito huo.

"Kwa upande wangu matatizo yalianza baada ya ujauzito kuharibika. Sijui upande wake lakini kwangu yalianza hapo. Nilibadilika tu. Nilipambana na hayo yote pekee yangu, sikusaidiana na mtu, nilikuwa pekee yangu," Muthoni alisema.

Mnamo mwaka wa 2020, Muthoni na Mulamwah walitengana kwa muda baada ya kupoteza mtoto kabla ya kuzaliwa. Hata hivyo hawakuweka bayana kilichokuwa kimewatenganisha.

Muthoni alifichua kuwa  kuharibika kwa mimba yake pia kulimletea hamu kubwa ya kupata watoto. Alisema daktari alimshauri apate mtoto ili kuweza kupata utulivu wa akili.

"Ukiharibikiwa na mimba, unachotaka baadae ni kupata mtoto. Hakuna uwezekana ifike mahali nitake kuavya ilhali nilitaka mtoto sana. Hata nilishauriwa na daktari nipate mtoto ili niwe sawa kiakili," Muthoni alisema.

Hivi majuzi Mulamwah alimshtumu mpenzi huyo wake wa zamani kwa kujaribu kutoa mimba ya miezi mitatu. Muthoni hata hivyo amepuuzilia mbali madai hayo huku akisisitiza alitamani sana kupata mtoto.