"Niruhusu nipumue kwanza," Diana Marua ashangazwa na mwanadada aliyechorwa tattoo ya sura yake

Muhtasari

•Diana alipakia tena picha ya tattoo ya mwanadada huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kusema kuwa amekosa maneno ya kumwambia.

•Waithera alipohojiwa alisema kuwa Diana ni role model wake na anatazamia kupatana naye siku moja.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA, ROSE WAITHERA

Mwanavlogu Diana Marua amesema kuwa ameshangazwa sana na hatua ya shabiki wake mmoja ya kuchorwa tattoo ya sura yake.

Hivi majuzi, Bi. Rose Waithera alionyesha tattoo ya sura ya Diana kwenye mgongo wake na kueleza jinsi anavyompenda msanii huyo. Waithera aliwaomba wanamitandao wamsaidie kumfikishia mke huyo wa Bahati ujumbe kuwa anamshabikia sana.

"Ananisaidia sana. Anatokea kuwa mwanadamu ninayempenda zaidi," Waithera aliandika chini ya picha ya tattoo yake mpya.

Hatimaye ujumbe wa Waithera ulimfikia Diana ambaye hivi majuzi alizinduliwa kama mwanamuziki akijitambulisha kama rapa Diana B.

Diana alipakia tena picha ya tattoo ya mwanadada huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kusema kuwa amekosa maneno ya kumwambia.

"Sina maneno. Rose Waithera niruhusu nipumue kwanza," Diana aliandika.

Waithera akiwa kwenye mahojiano na Nicholas Kioko alisema kuwa Diana ni role model wake na anatazamia kupatana naye siku moja.

"Dee mimi ni shabiki wako. Ningependa kukutana nawe ana kwa ana tuongee 1,2,3. Yeye ni role model wangu," Alisema.