Sarah Kabu afunguka kuhusu masaibu ya ndoa yake na mipango ya talaka

Muhtasari

•Sarah alisema alianza kumshirikisha mumewe kwenye mazungumzo ya utengano wa amani mapema mwaka huu baada ya kuchoshwa na maisha aliyokuwa anaishi.

•Sarah alikiri kwamba amekuwa akijua kuhusu watoto wengine wawili wa mumewe ambao alipata kutoka kwa mahusiano yake ya awali.

Sarah Kabu na Simon Kabu
Sarah Kabu na Simon Kabu
Image: HISANI

Mfanyibiashara mashuhuri Sarah Kabu amekiri kwamba ndoa yake na Simon Kabu haijakuwa imara kwa muda sasa.

Akiwa kwenye mahojiano na Tina Lewis, Sarah alifichua  kuwa mipango ya kutengana na mwazilishi huyo wa mwenza wa Bonfire Adventures imekuwa ikiendelea.

Sarah alisema alianza kumshirikisha mumewe kwenye mazungumzo ya utengano wa amani mapema mwaka huu baada ya kuchoshwa na maisha aliyokuwa anaishi.

"Tangu Januari nikifanya maazimio yangu ya mwaka mpya nilijiuliza kama nataka kuishi mwaka mwingine vile. Nilianza kuzungumza naye kuhusu utengano wa amani na kushirikiana katika malezi. Kilichonisumbua zaidi ni kuwa singependa kuvunjika kwa ndoa yangu kuchochee kuvunjika kwa ndoa zingine. Ni jambo ambalo nimekuwa makini sana kuhusu," Sarah alisema.

Aliongeza, "Nimekuwa nikimwambia sina raha sana kwa ndoa na nimechoka kudanganya. Tulikuwa tunazungumza. Nilitaka ushirikiano mzuri hata kwenye malezi"

Sarah alikiri kwamba amekuwa akijua kuhusu watoto wengine wawili wa mumewe ambao alipata kutoka kwa mahusiano yake ya awali.

"Alikuwa na mahusiano na mtu na wakapata binti. Akawa na mahusiano na mwingine na wakapata mtoto mvulana. Wakati tulikuwa tunafunga ndoa nilijua kuhusu hao. Tukiongea nilimwambia natumai watu hao hawaingilia ndoa yetu. Aliniahidi kuwa wako sawa walipo na hawataingilia. Amekuwa akiwasaidia kwa umbali," Alisema.

Hata hivyo alifichua kuwa siku za hivi majuzi mahusiano ya zamani ya mumewe yamekuwa yakitikisa ndoa yao.

Ndoa ya wafanyibiashara hao wawili imechukuliwa kama mfano mzuri na wengi. Hata hivyo, Sarah ameweka wazi kwamba ndoa hiyo yao ya takriban mwaka mmoja haijakuwa mteremko tu. Alisema wamepitia milima na mabonde mengi hadi kufikia hatua akahisi amechoka.

"Tumekuwa na nyakati nzuri. Kumekuwa na nyakati ambazo ameniumiza... Tumekuwa na masuala yetu kwa takriban miaka kumi. Ilikuja kujulikana hadharani nikiwa na msongo wa mawazo," Sarah alisema.