"Nisamehe Simon!" Sarah Kabu aomba msamaha kwa kufichua masaibu ya ndoa yake

Muhtasari

•Sarah amedai alikuwa amekumbwa na msongo wa mawazo katika kipindi ambapo alifichua masaibu ya ndoa yake.

•Mama huyo wa watoto wawili amemuomba msamaha mumewe na kumsihi wasuluhishe mizozo yao nje ya mitandao.

Sarah Kabu na mumewe Simon Kabu
Sarah Kabu na mumewe Simon Kabu
Image: HISANI

Mfanyibiashara Sarah Kabu amejuta matamshi ambayo amekuwa akitoa kuhusu ndoa yake na Simon Kabu.

Mwanzilishi huyo mwenza wa Bonfire Adventures amedai alikuwa amekumbwa na msongo wa mawazo katika kipindi ambapo alifichua masaibu ya ndoa yake.

"Poleni familia. Nilipokuwa nimekumbwa na msongo wa mawazo, nilisema mambo ambayo singesema mitandooni na inapotosha. Maisha ni somo na tunasoma kila siku," Sarah amesema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto wawili amemuomba msamaha mumewe na kumsihi wasuluhishe mizozo yao nje ya mitandao.

"Nisamehe Simon. Naomba tusuluhishe mambo yetu nje ya mtandao. Yote ni sawa. Tafadhali tuwekeni katika maombi. Ndoa hufanya kazi," Sarah alisema.

Akiwa kwenye mahojiano na Tina Lewis, Sarah alifichua  kwamba mipango ya kutengana na mumewe imekuwa ikiendelea.

Sarah alisema alianza kumshirikisha mumewe kwenye mazungumzo ya utengano wa amani mapema mwaka huu baada ya kuchoshwa na maisha aliyokuwa anaishi.

"Tangu Januari nikifanya maazimio yangu ya mwaka mpya nilijiuliza kama nataka kuishi mwaka mwingine vile. Nilianza kuzungumza naye kuhusu utengano wa amani na kushirikiana katika malezi. Kilichonisumbua zaidi ni kuwa singependa kuvunjika kwa ndoa yangu kuchochee kuvunjika kwa ndoa zingine. Ni jambo ambalo nimekuwa makini sana kuhusu," Sarah alisema.

Aliongeza, "Nimekuwa nikimwambia sina raha sana kwa ndoa na nimechoka kudanganya. Tulikuwa tunazungumza. Nilitaka ushirikiano mzuri hata kwenye malezi"

Sarah alikiri kwamba amekuwa akijua kuhusu watoto wengine wawili wa mumewe ambao alipata kutoka kwa mahusiano yake ya awali.

"Alikuwa na mahusiano na mtu na wakapata binti. Akawa na mahusiano na mwingine na wakapata mtoto mvulana. Wakati tulikuwa tunafunga ndoa nilijua kuhusu hao. Tukiongea nilimwambia natumai watu hao hawaingilia ndoa yetu. Aliniahidi kuwa wako sawa walipo na hawataingilia. Amekuwa akiwasaidia kwa umbali," Alisema.

Hata hivyo alifichua kuwa siku za hivi majuzi mahusiano ya zamani ya mumewe yamekuwa yakitikisa ndoa yao.

Ndoa ya wafanyibiashara hao wawili imechukuliwa kama mfano mzuri na wengi. Hata hivyo, Sarah ameweka wazi kwamba ndoa hiyo yao ya takriban mwaka mmoja haijakuwa mteremko tu. Alisema wamepitia milima na mabonde mengi hadi kufikia hatua akahisi amechoka.

"Tumekuwa na nyakati nzuri. Kumekuwa na nyakati ambazo ameniumiza... Tumekuwa na masuala yetu kwa takriban miaka kumi. Ilikuja kujulikana hadharani nikiwa na msongo wa mawazo," Sarah alisema.