"Naomba ukue na maarifa na hekima ili kuleta mabadiliko duniani," Gidi amsherehekea bintiye

Muhtasari

•Gidi ametaja siku ya kuzaliwa kwa bintiye  kama siku maalum  huku akimtakia hekima na maarifa zaidi anapoendelea kukua.

•Gidi amekuwa  akitumia likizo yake kuzuru maeneo mbalimbali ya Ulaya akiwa ameandamana na binti yake.

Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Mtangazaji wa Kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi Gidi Ogidi amesherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yake Marie-Rose.

Marie-Rose anaadhimisha miaka sita tangu alipozaliwa. Gidi ametumia siku hii kumhakikishia bintiye kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Ametaja siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa bintiye kama siku maalum sana  huku akimtakia hekima na maarifa zaidi anapoendelea kukua.

"Hii ndiyo siku ambayo Bwana ametengeneza. Marie-Rose anatimiza umri wa miaka 6 leo. Kheri za siku ya kuzaliwa nya Kanyamwa. Naomba ukue na maarifa na hekima ili kuleta mabadiliko katika dunia hii.Papa anakupenda," Gidi alimwandikia bintiye kupitia Instagram.

Mtangazaji huyo mahiri aliambatanisha ujumbe wake na picha maridadi ya binti huyo wake mpendwa.

Gidi amekuwa katika kipindi cha likizo tangu wiki iliyopita. Amekuwa akitumia fursa hiyo kuzuru maeneo mbalimbali ya Ulaya akiwa ameandamana na binti yake.

Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii mwanamuziki huyo wa zamani amekuwa akipakia video na picha zake na bintiye wakiwa maeneo mbalimbali ambayo wamezuru.

Picha zake za hivi karibu zinaashiria kuwa yupo nchini Ufaransa ambapo ameweza kukutana na baadhi ya marafiki zake na wafanyikazi wake wa zamani.

Gidi anatarajiwa kuungana tena na mtangazaji mwenzake Ghost katika kipindi chetu cha asubuhi hivi karibuni baada ya muda wake wa mapumziko kukamilika.

Kwa sasa kutoka Radio Jambo tunamtakia Marie-Rose kheri za siku ya kuzaliwa na vilevile tunamtakia Gidi likizo njema.