Enock Bella wa Yamoto Band afunguka suala la kuwaonea kijicho Mbosso na Aslay

Muhtasari

•Enock alisema kamwe hajawahi kumuonea kijicho Mbosso licha ya kuwa ameweza kupata mafanikio makubwa ya kimuziki zaidi yake na Aslay.

•Alisema hawajaweza kuwasiliana na Aslay kwa kipindi kirefu kwa vile kila mmoja wao yupo katika harakati za kutafuta riziki kivyake.

Wanabendi wa Yamoto; Mbosso, Beka Flavour, Aslay na Enock Bella
Wanabendi wa Yamoto; Mbosso, Beka Flavour, Aslay na Enock Bella
Image: HISANI

Mwanamuziki wa Bongo Enock Bellla ameweka wazi kuwa hakuna uhasama wowote kati yake na wanabendi wake wa zamani katika Yamoto Band, Aslay na Mbosso.

Akiwa kwenye mahojiano na Mbengo TV, Enock alisema wasanii hao wawili waliokuwa wanabendi wenzake ni kama wanafamilia yake.

Enock alisema kamwe hajawahi kumuonea kijicho Mbosso licha ya kuwa ameweza kupata mafanikio makubwa ya kimuziki zaidi yake na Aslay.

"Mbosso ni familia yangu hasa. Yeye ni sehemu yangu. Mimi na Mbosso ni sehemu ya familia kubwa. Mimi nipo kati, sina wivu kwa yeyote na haiwezi kutokea. Siwezi kugombana na mtu yeyote," Enock alisema.

Msanii huyo hata hivyo alikiri kuwa anatamani sana kupiga hatua kubwa za kimuziki kama zile alizopiga Mbosso.

Bella alisisitiza kuwa Mbosso ni nguzo muhimu sana katika taaluma yake ya muziki huku akifichua kuwa msanii huyo wa Wasafi huwa anamsaidia sana katika mambo mbalimbali yanayohusiana na muziki wake.

"Mimi namuombea daima na siwezi kumuonea chuki ama wivu isipokuwa nitatamani kupata njia bora na kubwa kama alizozipata yeye kuhakikisha muziki wake umefika pale. Wenzetu wametutangulia kwenye kufanya muziki wao kuwa biashara kubwa yenye mapato makubwa kwenye nchi. Hicho ndio kitu ambacho natamani... Vitu vyangu vingi ananisaidia Mbosso," Bella alisema.

Bella pia aliweka wazi kuwa uhusiano wake na Aslay ni mzuri. Hata hivyo alisema hawajaweza kuwasiliana na yeye kwa kipindi kirefu kwa vile kila mmoja wao yupo katika harakati za kutafuta riziki kivyake.

"Inafika miezi mitatu, minne hatujawasiliana. Yote ni kwa sababu kila mtu yupo kwenye harakati za kutafuta riziki. Ikitokea nahitaji kitu kutoka kwake kwa huu muda basi naweza nikampata kwa huu muda. Kutokana na sababu za kutafuta riziki imekuwa ngumu kukutana naye mara kwa mara," Alisema Bella.