"Tumeolewa na mume mmoja, tunapendana, hawezi oa mke wa 3" - Serah na Maureen kuhusu Abraham

Abraham ameoa wake wawili Serah na Maureen na wote wanapendana huku wakiamini hawezi oa mke wa 3.

Muhtasari

• "Sifikirii kama anaweza oa mke mwingine kwa sababu anaonekana ameridhika" - Serah

• "Naelewa yeye ni binadamu na siwezi jua kile anafikiria lakini kila mara nikimuangalia, ameonekana kuridhika na sisi wawili" - Maureen.

Serah, Maureen na mume wako Abraham
Image: Lynn Ngugi (YouTube screenshot)

Mwanaume mmoja kwa jina la Abraham katika siku za hivi karibuni amekuwa akigonga vichwa vya habari baada ya habari kuvuja kwamba ameoa wanawake wawili na wote wanapendana na kuheshimiana ambapo wanaishi pamoja bila chuki au mikwara inayoshuhudiwa katika familia nyingi zenye mfumo huo.

Wanawake hao ambao ni Serah na Maureen wanapendana kama marafiki na wake wa bwana Abraham ambapo watu wengi wamekuwa hawaamini kwamba ndoa ya wake wawili kuishi katika nyumba moja na kufanya mambo yao pamoja kama marafiki inawezekana.

Familia hiyo ya ajabu ikizungumza katika mahojiano na Lynn Ngugi walisema kwamba wanafurahia kuwa na mume mmoja na kufichua kwamba mapenzi yao hayaeleweki na watu lakini hilo haliwazuii hata kidogo kuendelea na mapenzi yao kwani hawana haja ya kusikiliza watu.

“Sina haja ya kuongeza mke wa tatu kwa sababu nimeridhika na hawa wake wangu wawili, bila shaka kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuilea familia hii. Kwangu mimi nimelenga tu mustakabali wa familia hii yangu na ninachokijua no kwamba ukitaka kufanikiwa lazima tu watu watakurushia mawe kutoka kila pande,” alisema Abraham alipoulizwa kama ana nia ya kuongeza mke wa tatu kama ambavyo wanamitandao wamekuwa wakisema.

Kwa upande wake Maureen, alisema kwamba anaelewa Abraham ni binadamu na kwamba haelewi nini huwa katika mawazo yake lakini akasema kwamba kila mara anapomuangalia tu anaona ni kama ameridhika na wao wawili na kusisitiza kwamba wote kama familia wamemakinika katika kulea familia yao na pia kuwekeza kwa ajili ya maisha ya kesho.

Serah ambaye ni mke wa kwanza kwa upande wake alisema pia hafikirii kabisa kwamba Abrahamu anaweza oa mke wa tatu.

“Sifikirii hivo. Sifikirii kama anaweza oa mke mwingine kwa sababu anaonekana ameridhika, ana furaha na pia ni mtu ametulia sana,” alisema Serah.

Maneno hayo yenye upendo mwingi kutoka kwa wake zake Abraham yalimgonga maskioni na kuingia moyoni ambapo alisimama katikati yao na kuwashika mkono na kusema kwamba jinsi ambavyo amesikia wakizungumza kutokana nyoyoni mwao basi upendo wa kweli umetaradadi katika familia yake.

“Nafikiri baada ya kila kitu ambacho nimesikia hapa na kwa kile mimi najua, ninaheshimika sana sana, nimenyenyekea sana, mimi ni mbarikiwa kuwa na nyinyi wote maishani mwangu. Ninaomba kuwa nitakuwa na uwezo wa kulinda heshima ile ambayo mmenipatia, nawapenda wote sana,” Abraham alimalizia.