Ringtone Apoko ajitolea kumpa Zari jumba la kifahari jijini Nairobi licha ya kukataliwa 2018

Alisema yupo tayari kumpa jumba lake ambalo alidai kipo katika mtaa wa Karen.

Muhtasari

•Ringtone sasa amejitolea kumpatia mwanasoshalaiti huyo moja ya nyumba zake za kifahari jijini Nairobi.

•Apoko alisema alikosa kukutana na Zari alipokuwa nchini mwezi uliopita kwa kuwa alikuwa bize na kazi zake.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO, ZARI HASSAN

Mwanamuziki maarufu Ringtone Apoko amedokeza kuwa bado anavutiwa na mwanasoshalaiti wa Uganda, Zari Hassan.

Mwaka wa 2018, msanii huyo ambaye hivi majuzi alitangaza mpango wa kugura sekta ya injili na kuanza kuimba nyimbo za mapenzi alikiri upendo wake mkubwa kwa mama huyo wa watoto watano.

Apoko aliandika ujumbe mrefu wa Instagram akitangaza mapenzi yake kwa sosholaiti huyo na kuahidi kutomuumiza kama Diamond.

"Mpendwa Zari, Najua unakuja Kenya wakati wowote kuanzia sasa. Nachukua fursa hii kukukaribisha katika nchi yangu ninayoipenda. Niliangalia na nikagundua kuwa ulikuwa kanisani ⛪ Jumapili nina furaha kwa sababu ni kwa Yesu pekee ambapo hutaumizwa kama Diamond alivyoumia," Aliandika mnamo Mei 10, 2018.

Katika juhudi za kumtongoza ili akubali ndoa naye, msanii huyo asiyepungukiwa na drama hata aliendelea kujitolea kumkabidhi Zari gari yake aina ya Range Rover Sport. Zari hata hivyo alipuuza juhudi zake na kubainisha kuwa hamtaki.

Ringtone sasa amejitolea kumpatia mwanasoshalaiti huyo moja ya nyumba zake za kifahari jijini Nairobi.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari alisema Zari hahitaji kutoa pesa zake kununua nyumba nchini Kenya kwani yupo tayari kumpa jumba lake ambalo alidai kipo katika mtaa wa Karen.

"Kama kweli anatamani kukaa Kenya, najitolea kumpa jumba bure. Sio eti kwa sababu nataka tuwe na mahusiano. Mimi apana. Zari nitampa jumba bure. Siwezi kumpa Runda, simtaki kwa sehemu yangu, Naweza kumpa Karen," Alisema.

Apoko alisema alishindwa kukutana na crush huyo wake alipokuwa nchini mwezi uliopita kwa kuwa alikuwa bize na kazi zake.

"Alikuja kipindi ambacho sikuwa na muda wa kufocus. Nilikuwa nafocus na mambo mengine. Nilisikia alikuwepo lakini sikupata muda wa ata kufuatilia mambo yake," Alisema.

Mwezi uliopita Zari alifanya ziara ya kikazi nchini Kenya  na kushuhudia  uzinduzi wa jumba  la kipekee ambalo limejengwa jijini Nairobi.

Alihojiwa ikiwa angependa kuishi Kenya katika miaka ya baadae hakutupilia mbali uwezekano huku akibainisha kuwa hapa ni kama nyumbani kwake pia.

"Sijui lakini kila kitu chawezekana. Mimi ni Mwafrika Mashariki, Kenya ni sehemu ya Afrika Mashariki. Chochote chaweza kutokea," Alisema.