Bifu? Nandy hatimaye ajibu madai ya kumlipa mtangazaji kumchafulia jina Zuchu

Nandy ameweka wazi kuwa kuna uhusiano mzuri kati yake na Zuchu

Muhtasari

•Nandy amepuuzilia mbali madai ya kumlipa mtangazaji na mchekeshaji Mwijaku ili  kumshambulia Zuchu.

•Nandy alimkosoa Mwijaku kwa kusisitiza kuwa alitafuta huduma zake katika vita vyake na Zuchu.

Nandy na Zuchu
Image: INSTAGRAM

Malkia wa muziki wa Bongo Faustina Mfinanga almaarufu Nandy amepuuzilia mbali madai ya kumlipa mtangazaji Mwijaku kumshambulia Zuchu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nandy aliweka wazi kuwa ana uhusiano mzuri na binti huyo wa Khadija Kopa.

Mke huyo wa Bilnass alidai kuwa hana ugomvi na msanii yeyote wala hana nia ya kumdhuru mwenzake yeyote.

"Mimi sio mtu wa kueleza mambo sana. Nishawahi kushambuliwa sana, hata nikielezea haitasaidia. Ata nikikaa kimya haitasaidia. Itapita tu kama yalivyopita mengine. Hata hivyo, mimi nina upendo na kila mtu na siko hapa kufanya mabaya kwa mtu yeyote yule. Tusaidiane. Kila mtu naongea naye vizuri," Alisema Nandy.

Nandy alidokeza kuwa hana mpango wa kufafanua zaidi kuhusu madai hayo na kuwaomba watu kuangazia muziki badala yaliyodaiwa.

Hata hivyo alimkosoa mtangazaji Mwijaku kwa kusisitiza kuwa alitafuta huduma zake katika vita vyake na Zuchu.

"Binadamu ndivyo alivyo. Nishawahi kumwambia (Mwijaku) kwamba malipo ni hapa hapa duniani. Ya Mungu ni hapa hapa duniani. Kama aliona vitu alivyofanya ni sawa, ni sawa. Lakini mimi siwezi kukaa na kuanza kueleza. Vitu ni vingi vya kufanya," Alisema.

Wiki jana klipu ya sauti iliyodaiwa kuwa mazungumzo kati ya Nandy na Mwijaku ilivunjishwa na kusambazwa mitandaoni.

Kwenye klipu hiyo,  aliyedaiwa kuwa Nandy alisikika akimpa maelezo aliyedaiwa kuwa Mwijaku kuhusu jinsi ambavyo angemchafua Zuchu.

“Halafu Mwijaku, kwenye kwamba walikuwa walikuwemo wasanii wangapi akiwemo Zuchu, andika hivi, hiyo hoja kwanza itoe na uandike hakuna mtu ambaye atapewa dili la hela nyingi, alikataa yeye, haswa suala la pombe. Isionekane hivo kwa sababu mtu atajua kwamba tumesema zaidi yaani tumefichua mbala maelezo ya ndani," Sauti iliyodaiwa kuwa ya Nandy ilisikika ikisema.

Baada ya klipu hiyo kusambaa Mwijaku alijitokeza kudai kuwa ni ya kweli na kusisitiza kuwa Nandy alikuwa na nia ya kumwangusha Zuchu.

Haya yalijiri miezi kadhaa baada ya Zuchu kudai kuwa alifuatwa na kampuni ya kuuza vileo ili kumpa dili ya kuwa balozi wa matangazo yao ya kibiashara ila akakataa kutokana na msimamo wake wa kidini.