Maelezo ya helikopta na ndege ya kibinafsi ya Diamond yafichuliwa

Idriss alisema kuwa ndege hiyo ilimgharimu Diamond dola milioni 520.

Muhtasari

•Idriss alifichua kuwa chopa hiyo ya Diamond ina injini mbili na ina uwezo wa kubeba takriban abiria wanane.

•Mtangazaji huyo pia alifichua kuwa ndege binafsi ya bosi wake tayari imewasili Tanzania.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Helikopta mpya ya kibinafsi ya bosi wa WCB Diamond Platnumz ilitengenezwa na kuagizwa kutoka Scotland.

Hii ni kwa mujibu wa mtangazaji maarufu wa Wasafi Media Idriss Kitaa ambaye alizungumza na Mbengo TV.

Idriss alifichua kuwa ndege hiyo ya Diamond ina injini mbili na ina uwezo wa kubeba takriban abiria wanane.

"Ina injini mbele na nyuma. Ina vitu vya watu wanane. Ni helikopta yetu sote. Ni helikopta kama zinazoonekana siku ya Uhuru," Idriss alisema.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha Mashamsham pia alifichua kuwa ndege binafsi ya bosi wake tayari imewasili Tanzania.

Alidai kuwa ndege hiyo ilimgharimu Diamond dola milioni 520 (Ksh 62B).

"Ina viti vya watu zaidi ya ishirini humo ndani. Ina mgahawa, ina choo, mabafu manne. Pia ina chumba cha kubadilishia nguo cha rubani mmoja," Alisema.

Idriss alifichua kuwa ndege hiyo pia ina mlinzi na chumba cha kufungia mtu anayezua vurugu mle ndani.

"Pia kuna matenki ya mafuta ambayo tunatembea nayo ndani ya ndege hiyo ya kibinafsi," Alisema.

Aliwakashifu wakosoaji ambao wamekuwa wakidai kuwa ndege ambayo staa huyo wa bongo alinunua ni mzee na imetumika kwingine.

Pia aliwakosoa walitilia shaka hatua ya msanii huyo kununua ndege.

Takriban wiki moja iliyopita Diamond alitangaza habari za kuwasili kwa helikopta yake kupitia ukurasa wake wa Instagram.

“Mungu ni mwema, nimenunua helikopta yangu leo,” aliandika kwenye Instastori.

Staa huyo wa Bongo alitangaza mpango wa kununua ndege ya kibinafsi takriban miezi mitatu iliyopita.

Diamond alifichua kuhusu mpango wake wakati akimtakia meneja wake El-Jefe Mendez heri za siku ya kuzaliwa.

"Tulinunua 2021 Rolls Royce Black Bedge Zero Kilometre mwaka jana, na tunanunua ndege ya kibinafsi mwaka huu!! hiyo ndio tafsiri ya kuwa na usimamizi bora!! Ni Siku ya Kuzaliwa ya meneja wangu Sallam Sk," Diamond aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.