Kampuni ya Transline yajitenga na klipu ya mfanyikazi wao akisherehekea kushindwa kwa Raila

Amkeni ameshindwa tena - Mfanyikazi huyo anaonekaan akisherehekea.

Muhtasari

• “Hatua za kinidhamu zimetekelezwa kwa mhusika na tunaomba radhi kwa wateja wetu" - Transline.

Kampuni ya usafiri imemfuta kazi jamaa aliyesherehekea ushinde wa Raila
Kampuni ya usafiri imemfuta kazi jamaa aliyesherehekea ushinde wa Raila
Image: Facebook//Transline

Jumatano kumekuwa na barua inayokisiwa kutoka kwa kampuni ya usafiri ya Transline nchini Kenya ikieleza kujitenga na video na mfanyikazi wao mmoja aliyeonekana kwenye video akisherehekea kutupiliwa mbali kwa ombi la Raila Odinga kutaka kubatilishwa kwa ushindi wa Ruto.

Sakata lilianza baada ya mahakama ya upeo kuithinisha ushindi wa Ruto na jamaa huyo mfanyikazi wa kampuni ya Trasnline alijirekodi kwenye video akisherehekea kushindwa kwa Raila kwa mara nyingine tena huku akipiga mbinja na kuwaita watu kuamka akisema kwamba (Raila) ameshindwa tena.

“Amkeni, ameshindwa tena,” mfanyikazi huyo wa Transline alionekana akipiga mbinja kwa mbwembwe.

Baada ya klipu hiyo kusambaa mitandaoni na kuzua mihemko mikali miongoni mwa wateja wa kampuni hiyo waliotafsiri kitendo hicho kama kampuni kusherehekea kushindwa kwa Odinga, Transline walijitokeza wazi na kukemea kitendo hicho huku wakijitenga na kusherehekea kwa mfanyikazi huyo.

Katika barua ambayo ilisambazwa kwenye mtandao wa Twitter na mtangazaji mmoja, Transline walimtambua jamaa huyo kama Cliff Onchiri ambaye ni mfanyikazi wao katika ofisi kuu jijini Nairobi na kusema wamekatisha mkataba wake mara moja.

“Kama kampuni tunataka kujitenga na klipu hiyo na kusema kwamba ilifanywa kwa utashi wa mtu binafsi na haiwakilishi maoni ya kampuni hata hivyo," sehemu ya barua hiyo ilisoma.

Walisema hata wao walishtushwa na klipu hiyo na kusema kwamba ilikuwa inalenga kuwaharibia jina kama kampuni na hata kuvuruga uhusiano wa kampuni na wafuasi wa Odinga ambao ni wateja wa kampuni hiyo kila siku.

“Hatua za kinidhamu zimetekelezwa kwa mhusika na tunaomba radhi kwa wateja wetu tunaowaenzi kutokana na chukizo lililosababishwa na klipu ile. Kama kampuni sisi tupo katika biashara na si katika siasa,” barua hiyo ilizidi kusoma.