Brenda Jons azungumzia safari yake ya wokovu

Mchekeshaji huyo amesema alipata umaarufu mkubwa baada ya kurudi kanisani.

Muhtasari

• Jons amesema kuwa aliweza kuupigania uhusiano wake na Mungu na kuweza kufaulu kujitoa kwenye dhambi ya uasherati.

•Jons alisema kuwa alikumbwa na matatizo na misukosuko katika safari yake ya wokovu baada ya Mungu kumchukua mtu aliyekuwa akimdhamini.

Brenda Jons
Image: Brendahjons Instagram

Mchekeshaji Brenda Gathoni almaarufu Brendah Jons ametoa ushuhuda kuhusu safari yake ya kanisa na mipango ya Mungu katika maisha yake.

Jons amesema kuwa aliweza kuupigania uhusiano wake na Mungu na kuweza kufaulu kujitoa kwenye dhambi ya uasherati.

Mchekeshaji huyo aliyejulikana kutokana na kauli 'Plesdent Kingston' amesema safari yake kwenye imani haijakuwa rahisi vile tangu aokoke miaka 13 iliyopita

"Miaka 13 iliyopita ndipo nilipoanza uhusiano wangu na Mungu kwa mara ya kwanza. Sikujua kilichomaanisha kuokoka lakini nakumbuka nikisema kuwa maisha yangu hayatakuwa kama yalivyokuwa tena,"alisema.

 Jons alisema miaka 8 baada ya kuokoka kwa mara ya kwanza Mungu alianza kumzawadi  na kumtumia kama kiumbe chake cha utakatifu.

Alisema alikuwa ameanza kusoma bibilia kwa sana kuliko alivyokuwa akiisoma hapo awali na hapo ndipo alipoona matunda ya kumtumikia Mungu.

Hata hivyo Jons alisema kuwa alikumbwa na matatizo na misukosuko katika safari yake ya wokovu baada ya Mungu kumchukua mtu aliyekuwa akimdhamini.

Mchekeshaji huyo alisema maswali yalizuka kuanzia hapo na ndipo alipoanza kujitenga na maombi na tumaini lake kwa Mungu likadidimia.

"Nilipompa Mungu maisha yangu nilijua ilimaanisha kuwa itabidi nijiweke kwenye mipango ya Mungu na kumtumikia kwa ukweli na kwa kiroho.Niliweza kuona mambo ambayo sikuwahi yaona hapo awali. Mungu alipomchukua mtu niliyekuwa nikimpenda nilishangaa kwani nilikuwa nikimtumikia yeye bila kusita, singewza kuelewa,"alisema.

Jons alisema akiwa katika chuo kikuu alijaribu kurudi kwenye njia ya wokovu ila alikuwa anashindwa mara kwa mara. Hata hivyo baada ya miaka michache aliweza kumrudia Mungu.

Alifichua kuwa baada ya kurudi kanisani, aliweza kupata umaarufu na ndipo alipoanza kuhubiri huku akiendelea kuchapisha mtandaoni.

"Mungu ameweza kunihamasisha kuongoza na kuongelea dhambi ya usherati. Watu wengi waliweza kuniongelesha kuhusu imani yangu akiwemo rafiki yangu wa dhati aliyeniambia kuwa mambo niliyokuwa nikiyapigania hadharani yatatumika kuiweka imani yangu kwenye majaribio,"alisema.

Jons alisema kuwa sasa ameweza kurudi kwenye maombi na kufungua ukurasa mpya.