Mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 24 azaa mapacha 5

Vyanzo vya habari viliripoti kuwa mwanafunzi huyo alipata ujauzito na kuzaa wakati wahadhiri wakiendelea na mgomo chuoni.

Muhtasari

• Mwanafunzi huyo kwa jina Oluomachi Linda Nwojo, aliwakaribisha watoto hao mwendo wa saa 9:02 usiku wa Jumatatu, Oktoba 3.

Msichana aliyezaa mapacha 5
Msichana aliyezaa mapacha 5
Image: Screengrab//Satellite

Mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu amegonga vichwa vya habari baada ya kuzaa watoto watano. Mwanafunzi huyo alibarikiwa na bahati hiyo ya kutokea kwa nadra mno huku mgomo wa wahadhiri wa vyuo vikuu ukiendelea nchini mwao.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa na Staelitte huko Nigeria, mwanafunzi huyo kwa jina Oluomachi Linda Nwojo, aliwakaribisha watoto hao mwendo wa saa 9:02 usiku wa Jumatatu, Oktoba 3.

Binti huyo wa miaka 24 alipata mapacha 5 wakiwemo wa kiume wawili na mabinti watatu, na ndio mara ya kwanza kutokea katika kituo hicho cha hospitali, kulingana na ripoti hiyo.

 Huku kampeni zikiwa zimepamba moto nchini Nigeria, vyanzo viliripoti kuwa mrengo fulani wa kisiasa uliingilia kati na kulipa bili ya hospitali ili mama huyo kuruhusiwa kutoka na watoto wake wote watano waliozaliwa salama salimini.

Hata kama kulikuwepo na mkanganyiko katika taarifa, baadhi ya watu walikuwa wanasema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa ameoleka haswa baada ya jamaa mmoja kuibuka kwenye mitandao na kupakia kuwa ni mkewe aliyezaa watoto hao mapacha 5.

Wengine walisema kuwa binti huyo alizungumza mwenyewe na kukanusha madai ya kuolewa, ambapo alisema kuwa yeye bado yupo singo ila akadinda kufichua mhusika wa mimba hiyo ya ajabu.