Video ya wanaume wakifanya kazi ya mjengo huku wakiimba kwa furaha imefurahisha mitandaoni

Wanaume hao walionekana wakipokezana saruji kutoka ghorofa ya chini kwenda juu huku wakicheza kwa furaha

Muhtasari

• Wow hii ni njia rahisi ya kufanya kazi kwa kupokezana kutoka chini kupanda ngazi, naipenda jamani - Kotei.

Hakuna kitu cha kutia moyo sana kama kumuona mtu anafanya kazi ambayo anaifurahia kuifanya kwa juhudi zake zote.

Video moja ya wafanyikazi katika eneo la mjengo wakifanya kazi kwa furaha huku wakiimba imefurahisha wanamitandao sana.

Video hiyo iliyopakiwa kwenye mtandao wa TikTok inawaonesha wafanyikazi hao vijana wakiwa wanakoroga saruji na kuirusha kwenda ghorofa za juu za mjengo huo ambao unaendelea huku wanaimba na kucheza kwa furaha.

Licha ya jua kali na kazi hiyo kuwa ngumu kwa wengi, vijana hao hawakuonekana kujutia kabisa katika kile walichokuwa wanakifanya kwani walikuwa wanafurahia kwa nyimbo nzuri, wakiwa wanajua fika kuwa mwisho wa siku ni sehemu ya riziki yake.

Kando na ishara yao ya furaha, pia walichukua mchanga hadi ghorofa ya mwisho kwa njia ya kuvutia. Badala ya kutumia karai au ndoo kupandisha saruji kwenye ngazi, walijenga vigingi viwili vya ziada na kuweka wanaume juu yake. Saruji hiyo ilikuwa inarushwa kwa vijiko vya kazini kutoka chini kabisa na kupokelewa na kikundi kingine kilichokuwa kwenye ghorofa ya kwanza, ambao pia wangewarushia wenzao wa juu na mwendelezo huo wa kupokezana kwa vijiko hadi kufika juu kabisa ulifurahisha watu walioitizama video ile.

“Wanaume kazini, Mungu aibariki kazi ya mikono yao katika jina la Yesu Amina,” mtumizi mmoja wa TikTok kwa jina Boniface Agu aliandika.

“Kazi na furaha,” Emmanuela Damahqua alisema.

“Wow hii ni njia rahisi ya kufanya kazi kwa kupokezana kutoka chini kupanda ngazi, naipenda jamani,” mwingine kwa jina Robert Kotei aliandika.

“Kufanya kazi kwa utimu kunafanya ndoto kutimia,” Braggey Dan aliandika.