(+video) Mfanyikazi wa mjengo asimamisha kazi kwa muda na kupiga magoti kuomba Mungu

Katika video hiyo, mwanaume huyo alidokeza kwamab hivyo ndivyo yeye hufanya kila anapohisi kuishiwa na nguvu.

Muhtasari

• “Muombaji ni mtu mwenye nguvu bwana awashe taa za mbinguni zikuangazie,” Sifoma Shifane alimhongera.

Kazi ya mjengo ni moja ya kazi ambazo zinaogopewa na wengi kutokana na ugumu unaozizingira, kutoka kuchanganya mchanga, maji na saruji ili mchanganyiko wa kujenga hadi kupandisha mchanganyiko huo kwa ngazi hadi ghorofa za juu.

Video moja ambayo imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii imewatia huruma wengi baada ya mwanaume mmoja kuonekana akikoroga mchanga na saruji kwa koleo na baadae kuanguka chini kwa magoti.

Katika video hiyo, mwanamume huyo alionekana akijaza mchanganyiko huo kwenye kontena la chuma kwa kutumia koleo.

Baada ya muda mfupi hata kabla kujaza kontena lile, alionekana kuachilia koleo kutoka mkononi na kuenda chini kwa magoti yake ambapo alionekana kama anapiga dua kwa kuomba sala kama Muumini wa dini ya Kiislamu vile.

Katika maneno ambayo aliandika kwenye video hiyo, mwanaume huyo kwa jina Raboi Janejan alidokeza kwamba huenda hiyo si mara ya kwanza anafanya hivyo kwani hufanya hivyo mara kwa mara pindi anapohisi kuishiwa na nguvu kutokana na kazi hiyo ngumu ya mjengo.

“Wakati siwezi stahimili hata zaidi,” Mwanaume huyo aliandika.

Watumizi wa Tiktok walioona video hiyo walishabikia jamaa huyo kwa kummiminia sifa kwa kuwa mtu muombaji sana.

“Muombaji ni mtu mwenye nguvu bwana awashe taa za mbinguni zikuangazie,” Sifoma Shifane alimhongera.

“Nakumbuka nilipokuwa nikifanya kazi ya ujenzi huko Nyeri. Nilikuwa nimetengenga chumba kimoja kama cha kuabudia. Wakati wa mapumziko ya chakula cha mchana nilikuwa nikienda huko na kusali. Mungu alifanya hivyo,” Wa Njeri alikumbuka.

“Mradi humfanyii mtu jambo lolote baya hakika Mungu atakubariki. Subiri wakati wako unakuja. Upendo na mwanga,” Mwingine alimwambia.