Magix Enga afunguka jinsi alivyoathirika baada ya kudai ni mwanachama wa Illuminati

Msanii huyo alidai alijiunga na Illuminati akiwa na umri wa miaka 23 akikusudia kuinua taaluma yake ya usanii.

Muhtasari

•Enga aliwashangaza Wakenya wengi baada ya kukiri hadharani kuwa mafanikio yake makubwa katika taaluma ya muziki yamewezeshwa na Illuminati.

•Enga sasa  anadai kuwa mara nyingi alipokuwa akifanya mahojiano kama hayo alikuwa amelewa na dawa za kulevya.

Image: INSTAGRAM// MAGIX ENGA

Mwanamuziki na Mtayarishaji wa Muziki mashuhuri nchini Kenya Magix Enga amekiri kwamba anajuta kudai kuwa ni mwanachama wa madhehebu maarufu ya kimataifa yanayohusishwa na ibada ya shetani, Illuminati.

Mapema mwaka huu, mwimbaji huyo mwenye umri wa ujana aliwashangaza Wakenya wengi baada ya kukiri hadharani kuwa mafanikio yake makubwa katika taaluma ya muziki yamewezeshwa na dhehebu hilo.

Katika mahojiano, Enga alidai alijiunga na Illuminati akiwa na umri wa miaka 23 akikusudia  kuinua taaluma yake ya usanii.

"Kila mwezi nilipokea pesa. Kuna gari fulani ilikuwa inakuja naambiwa niingie. Nilikuwa nakalia kiti cha nyuma lakini sikuwa naangalia ni nani anaendesha. Ningechukua pesa zangu kisha narudi studioni. Nilikuwa napata pesa  nyingi. Mfuko huo haukukosa  kitu kama milioni tano, wakati mwingine nilipata milioni saba. Ilikuwa pesa nyingi, nililala juu ya pesa," Enga alisema katika mahojiano na Presenter Ali.

Msanii huyo hata hivyo sasa amejitenga na madhebehu hayo na kuweka wazi kuwa madai hayo yalikuwa ya uwongo.

Enga sasa  anadai kuwa mara nyingi alipokuwa akifanya mahojiano kama hayo alikuwa amelewa na dawa za kulevya.

"Ilikuwa ni shinikizo la rika na ujinga mwingi. Hakuna kitu kama Illuminati. Mimi siamini hiyo," alisema katika mahojiano na Eve Mungai.

Mtayarishaji huyo alisema mafanikio yake makubwa katika tasnia ya muziki yamechangiwa zaidi  na bidii kubwa na kujituma kwake.

Alifichua kuwa mahojiano hayo yalichafua jina lake kiasi kwamba imekuwa vigumu kwa watu kuuchukulia muziki wake safi kwa uzito.

"Ningeomba mahojiano hayo yafutwe. Yakifutwe itakuwa jambo bora kwa sababu kwa sasa nafanya kazi safi," alisema.

Enga alifichua kuwa baada ya kufanya  mahojiano yale alipokea simu nyingi kutoka kwa watu ambao walitaka kuelezwa jinsi ya kujiunga na Illuminati.

"Mimi hushindwa nitawaambia nini. Nikiwaambia nilikuwa nimelewa watacheka tu. Hii kitu haiko, huwa nasikia tu na kuona kwa TV," alisema.

Mtayarishaji huyo amesema kuwa  tayari ameacha mihadarati na mambo mengine mabaya aliyokuwa akijihusisha nayo siku za hapo nyuma. Amedai kuwa kwa sasa anaangazia kufanya muziki safi tu.