Maoni: Harmonize riziki yake ni muziki, kutoa ngoma baada ya nyingine ndio ugali wake

Watu hawafai kulalamika kwamba ameachia albamu wakati bado wasanii wake wana albamu mpya sokoni kwani asilimia kubwa ya maisha yake hutegemea huo muziki.

Muhtasari

• "Mtu maisha yake yanaendeshwa na muziki. aani mnataka muziki wake uende jinsi mnavyotaka nyinyi, mwacheni mwana apambanie ugali wake." - maoni ya mdau.

Harmonize kwenye picha za awali akizindua albamu yake Made For Us
Harmonize kwenye picha za awali akizindua albamu yake Made For Us
Image: Instagram

Msanii Harmonize kutoka lebo ya Konde Music Worldwide Jumanne alitangaza kuachia albamu yake nyingine ‘Made for Us’, miezi kadhaa baada ya kuachilia albamu yake ya pili iliyokwenda kwa jina ‘Highschool’

Itakumbukwa uzinduzi huu wa albamu unafuatia albamu ya msanii wake katika lebo hiyo, Ibraah aliyeachia yake mwezi Juni mwaka huu kwa jina ‘The King of New School’, na wadau wengi katika tasnia ya muziki walihisi Harmonize hakufanya vizuri kuachia albamu yake wakati kuna albamu mpya ya msanii wake ambayo bado inang’ang’ana kutusua sokono.

Baadhi walihisi kana kwamba msanii huyo anajaribu kushindana na wadogo zake ndani ya lebo ya Konde Gang na kumshtumu kwa kile walisema kwamba angechukua muda kuzitangaza kazi za wasanii wake, haswa albamu mpya ya Ibraah kabla ya kuachia yake pia kwa sababu takribani mwaka mmoja uliopita tayari alikuwa ameachia albamu yake nyingine.

Harmonize mpaka sasa ana albamu tatu tangu atambulishwe rasmi kweney muziki, ya kwanza ikiwa Afro East, akaja akawabariki mashabiki wake kwa albamu ya Highschool na sasa hii ya Jumanne ya Made for Us.

Licha ya kusutwa kuwa anajaribu kushindana na wasanii wake, kuna baadhi ya wadau ambao walitolea maoni komavu sana na kumpongeza kwa juhudi zake kutoka muziki juu ya mwingine kila uchao bila kulala. Wenye maoni sawia na hayo walisema kuwa Harmonize riziki yake inatokana na muziki na hakuna hatia akiachia miziki kwa kufuatana mfululizo.

“Mtu maisha yake yanaendeshwa na muziki. Unataka asitoe albamu au nyimbo, unataka ale wapi? Mambo yake yaende vipi? Yaani mnataka muziki wake uende jinsi mnavyotaka nyinyi, mwacheni mwana apambanie ugali wake. Kutoa ngoma baada ya nyingine ndio ugali wake,” mkereketwa mmoja kwa jina Tin Martin aliandika kwenye Twitter.

Jamaa huyo pia alipinga vikali wale waliokuwa wanamkejeli Harmonize kwa kuzitaja baadhi ya ngoma ambazo tayari ameziachia kwenye albamu yake mpya.

“Kwahio Nyimbo zikiwa zishatoka ndo hazifai kuwa kwenye Album 😂😂😂😂😂😂 wee jamaa una chekeshaa umeongea pumba aseh. Mtu maisha yake yana endeshwa na music's unataka asitoe nyimbo/album unataka ale ninii 😂 unafikiri kutumia makalio ama?” Martin alipandwa na jazba.