"Siwezi kuvumilia tena!" Nyota Ndogo alalamika kuambukizwa kukoroma na mumewe mzungu

Msanii huyo amefichua amekuwa akikoroma kwa nguvu hadi kufikia hatua ya kujiamsha na kelele zake .

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili alilalamika kwamba huenda alipata tabia hiyo kutoka kwa mume wake Henning Nielsen.

•Sasa anatafuta kuelewa kiini cha tatizo hilo ambalo anadai mumewe amekuwa nalo kwa miaka mingi.

Henning Neilsen na Nyota Ndogo
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwimbaji Nyota Ndogo ni mwanamke mwenye wasiwasi baada ya kupata tabia za kukoroma ambazo hakuwa nazo hapo awali.

Kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto wawili alilalamika kwamba huenda alipata tabia hiyo kutoka kwa mume wake Henning Nielsen.

Alifichua kwamba siku za hivi majuzi amekuwa akikoroma kwa nguvu hadi kufikia hatua ya kujiamsha na kelele zake .

"Kuna siku huku nikiwa kwa gari la moshi tulikuwa tumekaa naangaliana na wazungu kisha nikasinzia nilikoroma koroma moja kubwa nikashtuka nikifungua macho nikapata wananiangalia wakaanza kucheka," aliandika chini ya picha  yake  na mumewe wakiwa ndani ya gari ya moshi ambayo alipakia.

Nyota Ndogo alisema alihisi aibu sana baada ya kukoroma miongoni mwa abiria na kukiri tukio hilo lilizua wasiwasi mkubwa ndani yake.

Sasa anatafuta kuelewa kiini cha tatizo hilo ambalo anadai mumewe amekuwa nalo kwa miaka mingi.

"Nauliza tu maana baba (mume) anakoroma huyu mpaka huwa nauamsha. Hivi atakuwa  kaniambukiza? Na kama ni kweli nataka iniondokee maana siwezi kuvumilia tena," alisema mwanamuziki huyo.

Nyota Ndogo na Bw Neilsen wamekuwa kwa ndoa kwa takriban miaka minane. Ingawa wawili hao hawaishi pamoja, mzungu huyo kutoka Denmark amekuwa akimtembelea Nyota humu nchini mara kwa mara.

Miezi michache iliyopita msanii huyo mkongwe alifichua kuwa alikutana na Bw Neilsen nchini Marekani. Alifichua kuwa aliishia kuchumbiana na mzungu huyo baada ya kutoridhishwa na mahusiano yake ya awali na wanaume wa Kiafrika.

Pia aliweka wazi kuwa hakujitosa kwenye mahusiano na mzungu huyo  kwa minajili ya kutosheleza kiu cha mahaba.

"Mimi niliteseka sana na Waafrika. Sio kuteseka umaskini lakini mapenzi. Hapa ndio nimepata mapenzi pesa mbona natafuta mwenyewe," alisema.

Hapo awali Nyota Ndogo alikuwa kwenye ndoa nyingine ambayo ilikosa kufua dafu. Ana watoto wawili kutokana ndoa yake ya kwanza.

Mapema wiki hii mwimbaji huyo alikataa zawadi ya iPhone 14 kutoka kwa mumewe na kusisitiza ameridhika na simu yake mzee.

"Niko na iPhone 11. Hiyo imenitosha. Ninaweza nikapiga picha, ninaweza nikapiga simu na tunayewasiliana naye anisikie," alisema katika video ya mazungumzo yake na mumewe ambayo alipakia Instagram.

Bw Neilsen hata hivyo alisisitiza kuwa simu ya mke wake ni mzee sana na alifaa kupata toleo jipya la iPhone.

Badala ya simu hiyo inayokadiriwa kugharimu takriban shilingi robo milioni, Nyota Ndogo alimshauri kununua kipande cha shamba nchini Kenya ili wajenge hoteli kama uwekezaji wa siku zijazo.

"Sitaki ukistaafu uje Kenya kuhangaika, tutakuwa na hoteli yetu," mwimbaji huyo alimwambia mumewe.

Mdenmarki huyo alionekana kukubali ushauri huo ila akasisitiza kuwa pamoja na kuwekeza, mkewe alihitaji simu mpya.