Sababu ya Nyota Ndogo kukataa zawadi ya iPhone 14 kutoka kwa mumewe mzungu

Bw Neilsen alisisitiza kuwa simu ya mkewe ni mzee na alifaa kupata toleo jipya la iPhone.

Muhtasari

•Nyota Ndogo alikataa ofa ya mumewe na kusisitiza kuwa aliridhika na iPhone ya toleo la zamani aliyokuwa nayo.

•Msanii huyo alimshauri mumewe kununua kipande cha shamba nchini Kenya ili waweze kujenga hoteli kama uwekezaji wa siku zijazo.

Bw Henning Neilsen na mkewe Nyota Ndogo
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Jumatatu mwanamuziki mkongwe Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo alichapisha video ya mazungumzo yake na mumewe Henning Nielsen.

Katika video hiyo iliyopakiwa kwenye Instagram, wanandoa hao walionekana wamekaa pamoja huku Bw Nielsen akipekua kwenye kompyuta yake.

Muda si muda, Nyota Ndogo ambaye alikuwa ameshika bakuli la vitafunwa alimuhoji mumewe kuhusu kile alichokuwa akifanya.

"Naangalia iPhone 14. Nataka kukununulia," Bw Neilsen alijibu.

Msanii huyo mzaliwa wa Pwani hata hivyo alikataa ofa ya mumewe na kusisitiza kuwa aliridhika na iPhone ya toleo la zamani aliyokuwa nayo.

"Niko na iPhone 11. Hiyo imenitosha. Ninaweza nikapiga picha, ninaweza nikapiga simu na tunayewasiliana naye anisikie," alisema.

Bw Neilsen ambaye ni mzaliwa wa Denmark alisisitiza kuwa simu ya mkewe ni mzee na alifaa kupata toleo jipya la iPhone.

Badala ya simu hiyo inayokadiriwa kugharimu takriban shilingi robo milioni, Nyota Ndogo alimshauri mumewe kununua kipande cha shamba nchini Kenya ili waweze kujenga hoteli kama uwekezaji wa siku zijazo.

"Sitaki ukistaafu uje Kenya kuhangaika, tutakuwa na hoteli yetu," mwimbaji huyo alimwambia mumewe.

Mdenmarki huyo alionekana kukubali ushauri huo ila akasisitiza kuwa pamoja na kuwekeza, mkewe alihitaji simu mpya.

iPhone 14 ndiyo toleo jipya zaidi la simu za Apple na kwa sasa inagharimu kati ya shilingi laki mbili na laki tatu hapa nchini Kenya.

Nyota Ndogo na Bw Neilsen wamekuwa kwa ndoa kwa takriban miaka minane. Ingawa wawili hao hawaishi pamoja, Mdenmarki huyo amekuwa akimtembelea Nyota hapa nchini mara kwa mara.

Mapema mwaka huu mwanamuziki huyo mkongwe alifichua kuwa alikutana na Bw Neilsen nchini Marekani. Alisema aliishia kuchumbiana na mzungu huyo baada ya kutoridhishwa na mahusiano yake na wanaume wa Kiafrika.

Pia aliweka wazi kuwa hakujitosa kwenye mahusiano na mzungu huyo  kwa minajili ya kutosheleza kiu cha mahaba.

"Mimi niliteseka sana na Waafrika. Sio kuteseka umaskini lakini mapenzi. Hapa ndio nimepata mapenzi pesa mbona natafuta mwenyewe," alisema.

Hapo awali mwanamuziki huyo kutoka Pwani alikuwa kwenye ndoa nyingine ambayo ilikosa kufua dafu. Ana watoto wawili kutokana ndoa yake ya kwanza.