Diamond ajivunia Rayvanny kujiunga na klabu ya mabilionea

Rayvanny aliwashukuru mashabiki wake kwa kuwezesha mafanikio yake makubwa.

Muhtasari

•Bosi huyo wa Next Level Music alipata dili hilo miezi michache tu baada ya kuondoka WCB na kuwa msanii wa kujitegemea.

Rayvanny na Diamond
Image: MAKTABA

Siku ya Jumatatu, staa wa Bongo, Rayvanny alisaini mkataba wa mamilioni na kampuni ya kusambaza muziki ya Afrika Kusini, Zikii Media.

Bosi huyo wa Next Level Music alipata dili hilo miezi michache tu baada ya kuondoka WCB na kuwa msanii wa kujitegemea.

Alitangaza habari hizo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo alichapisha picha zake akisaini mkataba huo.

"Mama mwanao ni bilionea Sasa !! Nina furaha sana kusaini dili langu kubwa la kwanza la Usambazaji duniani na familia yangu @mziiki. MAMA MWANAO NI BILIONEA SASA," alisema kwenye Instagram.

Mtunzi huyo wa kibao 'Number One' alimshukuru Mungu na mashabiki wake kwa kuwezesha mafanikio yake makubwa.

"Asante Mungu, asante sana mashabiki wangu wote kwa kuniunga mkono. Jiandae kwa Chui nakuja @ziiki_southside,"

Wanamitandao wengi wakiwemo watu mashuhuri walimiminika kwa chini ya chapisho la staa huyo kumpongeza kwa ushindi huo.

"Vanny Booooy, karibu kwenye Klabu ya Bilionea! 🔥👑" alisema Diamond.

Mapema mwaka huu Rayvanny aligura na lebo ya Diamond WCB na kujitosa katika kuzingatia lebo ya Next Level Music.

Rayvanny alikuwa chini ya usimamizi wa WCB kwa kipindi cha takriban miaka sita kabla ya kuchukua hatua ya kuondoa mwezi Julai. 

Wakati akitangaza kuondoka kwake, alishukuru uongozi mzima wa lebo hiyo ukiongozwa na Diamond ambaye amekuwa mwandani wake kwa kipindi kirefu.

“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja.. Shukrani za dhati kwa familia yangu Wasafi lakini pia kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” Alisema.

Hata hivyo,  ilidaiwa kuwa staa huyo alilazimika kulipa pesa taslimu Tsh800M (40.5) kabla ya kuondoka WCB.

Ripoti kutoka Bongo zilidai hangeweza kufanya shoo yoyote hapo awali kabla ya kutimiza madai aliyopatiwa.