Muigizaji Selina azungumzia hali ya ndoa yake na maendeleo ya bintiye mchanga

Muigizaji huyo alifichua kuwa kwa sasa mumewe anaangazia miradi mbalimbali ya muziki.

Muhtasari

•Muigizaji huyo ameweka wazi kuwa ndoa na familia yake ndogo na mwimbaji Phil Kimemia inaendelea vizuri.

•Aidha alisema tayari amerejea katika kazi yake ya uigizaji baada ya kujifungua miezi kadhaa iliyopita.

Phil Kimemia na Celestine Gachuhi
Image: INSTAGRAM// PHIL KIMEMIA

Muigizaji mashuhuri Celestine Gachuhi almaarufu Selina, kutokana na kipindi cha 'Selina' kwenye Maisha Magic East ameweka wazi kuwa ndoa yake na mwimbaji Phil Kimemia inaendelea vizuri.

Katika mahojiano na SPM Buzz, malkia huyo wa uigizaji pia alibainisha kuwa mtoto wao anaendelea kukua vizuri.

“Familia iko fiti. Mtoto ako sawa. Tunakua. Namshukuru Mungu sana. Mume ako sawa, Phil Kimemia ako sawa,” alisema.

Muigizaji huyo alifichua kuwa kwa sasa mumewe ambaye pia ni msanii anaangazia miradi mbalimbali ya muziki.

Aidha alisema tayari amerejea katika kazi yake ya uigizaji baada ya kujifungua na kufichua kwamba siku za hivi majuzi amehusika katika filamu mbalimbali ikiwa ni pamoja na za nje ya nchi.

 “Nafanya filamu fulani ambayo itaachiwa hivi karibuni ambayo nafurahia sana kuwa mhusika. Ni ya Kenya.” alisema.

Pia alifafanua zaidi kuhusu  ziara yake ya kikazi ya hivi majuzi katika nchi jirani ya Tanzania.

“Nilienda Tanzania takriban miezi miwili iliyopita kufanya series inayoitwa Yalaiti. Ni series inayoendelea. Ilikuwa sawa. Watanzania walinifanyia vizuri na kusherehekea yale ninayofanya. Nilifurahia sana”

Celestine alipoulizwa iwapo angewahi kufikiria kuhamia Tanzania katika siku za usoni, alisema;- "Nyumbani ndio bora. Acha nikae nyumbani. Lakini nikihitajika kuenda kufanya kazi kule nitaenda. Ndoto ni kufika Hollywood,"

Muigizaji huyo na mpenzi wake Phil Kimemia walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza pamoja mwishoni mwa mwezi Aprili.

Huku wakitangaza kuzaliwa kwa binti wao takriban wiki moja baadae, Celestine alisema kuwa kuzaliwa kwa mtoto huyo kulibadilisha maisha yake na ya mumewe kabisa. 

"Hata miujiza huchukua muda kidogo 😍,Binti wetu wa muujiza alikuja 😍❤️, ni wiki sasa imepita na maisha yetu yamebadilika kabisa❤️❤️🙏🙏 Phil Kimemia, namshukuru Mungu kwa ajili yako, umesimama nami tangu siku ya kwanza, katika heka heka, kama kuhani wangu. Mungu akubariki," alisema.

Bw Kimemia kwa upande wake alisema kuzaliwa kwa binti wao kulijenga upendo mkubwa zaidi kati yake na mkewe. Alisema bintiye ni zawadi kutoka juu na kudai kuwa sauti ya kilio chake punde baada ya kuzaliwa ndiyo sauti nzuri zaidi amewahi kusikia.

"Hatimaye nimekutana na msichana ambaye ana sauti nzuri zaidi duniani! Siwezi kamwe kusahau hisia hiyo niliposikia ukilia, ilikuwa sauti ya kipekee zaidi, nzuri sana," alisema.

Wawili hao walianza kuchumbiana baada ya kukutana kwa mara ya kwanza mwaka wa 2017.