Eric Omondi akosolewa kwa kurekodi mpenziwe akilia kwa uchungu baada ya ujauzito kuharabika

Mchekeshaji huyo alimrekodi Lynne akiomboleza baada ya kumpoteza mtoto wao akiwa tumboni.

Muhtasari

•Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Eric alichapisha video ambayo ilirekodiwa Jumatatu jioni ikimuonyesha mpenzi wake akilia kwa uchungu baada ya ujauzito wake kuharibika

•Baadhi wamesema kuwa kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na hakifai.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi amekuwa gumzo tena katika siku mbili zilizopita baada ya kurekodi kipindi cha huzuni cha yeye na mpenzi wake Lynne wakiomboleza baada ya kumpoteza mtoto wao akiwa tumboni.

Jumanne jioni, mchekeshaji huyo aliyezingirwa na utata mwingi alitangazia ulimwengu kuhusu tukio hilo mbaya lililowapata. Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Eric alichapisha video ambayo ilirekodiwa Jumatatu jioni ikimuonyesha mpenzi wake akilia kwa uchungu baada ya ujauzito wake kuharibika

Katika maelezo ya video hiyo, Eric alieleza kwamba juhudi zao nyingi za kuokoa maisha ya binti yao asiyezaliwa hazikuzaa matunda. Alieleza huzuni yake kubwa kwa kutokutana na binti yake waliyemtarajia sana.

"Jana usiku (Jumatatu)  ilikuwa moja ya usiku Mrefu zaidi maishani mwangu😥😥 Tulipigana kwa zaidi ya masaa 5 kujaribu kumuokoa Malaika wetu mdogo lakini Mungu alikuwa na mipango mingine. Hatukuwahi kukutana nawe lakini hakika tulikuhisi na tutakupenda Milele 🕊," aliandika chini ya video aliyopakia.

Pia alimfariji mpenzi wake Lynne na kuwapongeza wanawake kwa ujasiri wanaoonyesha katika nyakati kama zile.

Wanamitandao wamejitokeza kwa wingi kuwafariji wapenzi hao na kuwatia nguvu katika kipindi kigumu wanachopitia. Kundi kubwa la wanamitandao hasa watumizi wa Twitter wamejitokeza kuonyesha kusikitishwakwao na kitendo cha mchekeshaji huyo kurekodi matukio baada ya ujauzito kuharibika.

Baadhi wamesema kuwa kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na hakifai.

@droid254: "Namuonea huruma sana Eric Omondi. Kupoteza mtoto inasikitisha sana 💔 lakini je ni lazima angerekodi ili kupakia Instagram?" @droid 254 alisema kwenye Twitter.

@luhya_kidd: "Jambo la kuhuzunisha na kusikitisha zaidi ambalo nimeona leo kwenye mtandao ni Eric Omondi akiweka video yake na mkewe wakilia kando ya kitanda baada ya kumpoteza mtoto wao."

@Lsankei: Natumai mpenzi wa Eric Omondi atamwacha. Je unamrekodi vipi mwenzako akiharibikiwa na MIMBA na kupakia walimwengu waone??

@Rozay_Kamau: Kwa udadisi tu: Kwa nini Eric Omondi alikuwa akimrekodi mpenzi wake akiharibikiwa na mimba ili kupata maudhui ya Instagram?? Kuna vitu vya kuhuzunisha na vya faragha nisingependa kuendelea kurudi mitandaoni kutazama tena!"