Nameless afurahi baada ya kukutana na mwanadada anayefanana na mkewe Wahu (+picha)

Mwanadada huyo alifurahi kumuona Nameless na kumwambia mara nyingi watu humwambia anafanana na Wahu.

Muhtasari

•Wawili hao walikutana katika ukumbi wa Century Cinemax, katika Sarit Center ambapo Nameless alikuwa amehudhuria uzinduzi wa Filamu ya Black Panther.

•Msanii huyo alisema alifurahi sana kukutana na mwanadada huyo na kudokeza kuwa kukutana na mashabiki wake kila mara humpa motisha kufanya zaidi.

Image: FACEBOOK// NAMELESS

Alhamisi jioni, mwanamuziki mkongwe David Mathenge almaarufu Nameless alikutana na mwanadada anayefanana na mkewe Wahu Kagwi.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Baba huyo wa mabinti watatu alichapisha picha kadhaa za mkutano wake na mwanamke huyo ambaye alifurahi kumuona na kumwambia mara nyingi watu humwambia anafanana na Wahu.

Wawili hao walikutana katika ukumbi wa Century Cinemax, katika Kituo cha Biashara cha  Sarit, Westlands ambapo Nameless alikuwa amehudhuria uzinduzi wa Filamu ya Black Panther.

"Nilipotoka nje ya ukumbi wa sinema kwenda kujisaidia, nilikutana na mtu ambaye alifurahi kukutana nami kwa sababu watu humwambia kuwa anafanana na Wahu .Kwa hivyo tuliamua kupiga picha kwa furaha. Kwa kweli anafanana na mama Shiru,  ama naona vitu zangu 🧐🤔. Hata kisogo😳. Nilidhani chakula cha Shiru ametoroka Shiru Tena 😂😂😂 kumbe ni mtu anafanana naye😊🙌🏾🙌🏾," Nameless alisema chini ya picha zake na mwanadada huyo ambazo alichapisha.

Msanii huyo alisema alifurahi sana kukutana na mwanadada huyo na kudokeza kuwa kukutana na mashabiki wake kila mara humpa motisha kufanya zaidi.

"Usiwahi kuona  haya kuja nilipo  ili tupige picha, siwezi kukataa kunasa matukio kwenye picha na kutengeneza kumbukumbu,' aliwaambia mashabiki wake.

Nameless alikuwa ameandamana na bintiye mkubwa Tumiso Mathenge kwenye uzinduzi wa sinema ya Black Panther. Mke wake Wahu labda alikuwa ameachwa nyumbani akimtunza mtoto wao mchanga Wanjiru Mathenge.

Baada ya uzinduzi huo mwimbaji huyo alifichua kwamba ilimbidi kwanza amtie moyo bintiye ambaye mwanzoni aliogopa kukutana na watu wengine maarufu waliokuwa wamefika katika ukumbi huo

"Tumi aliogopa kukutana na watu fulani anaowapenda lakini nilimwambia atulie, ni watu kama yeye, wenye hofu kama zake! Kwamba tu walishinda baadhi ya hofu zao, Kuanguka na makosa ... Pia wewe utaweza!" alisema.

Nameless na Wahu wamekuwa pamoja kwa zaidi ya mwongo mmoja na wamebarikiwa na mabinti watatu pamoja; Tumiso, Nyakio na Wanjiru.