Karen Nyamu azungumzia kurudiana na mzazi mwenzake, Samidoh

Seneta huyo alidokeza kwamba Samidoh ndiye alifanya aache kuvaa wigi.

Muhtasari

•Karen alionyesha video yake ya kumbukumbu akiwa mjini Mombasa huku akiwa amevalia wigi kichwani na kudokeza kwamba aliacha kuzivaa baada ya kukutana na Samidoh.

•Karen alimjibu, "nikirudi uniite kang’ethe!"

Karen Nyamu na mzazi mwezake Samidoh
Karen Nyamu na mzazi mwezake Samidoh
Image: Instagram

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alitangamana na mashabiki wake kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatano.

Wakili huyo aliwajibu baadhi ya wafuasi wake ambao waliandika maoni chini ya chapisho moja ambalo lilionekana kumzungumzia baba ya watoto wake wawili wa mwisho Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Katika chapisho hilo la Jumatano, Karen alionyesha video yake ya kumbukumbu akiwa mjini Mombasa huku akiwa amevalia wigi kichwani na kudokeza kwamba aliacha kuzivaa baada ya kukutana na Samidoh.

"Hii ni miaka michache nyuma kwenye mkutano wa kisiasa mjini mombasa. Kabla nikutane na ka mtu kakaniambia vile kanachukia wigi nikazitupa mbali hahaha wacha tu nicheke sababu siwezi lia," Karen aliandika.

Wakati akimjibu shabiki mmoja, aliweka wazi kuwa alisikiliza alichoambiwa na mwanaume huyo na hata akaandika.

Mtumiaji mwingine wa Instagram alimbainishia seneta huyo kwamba hatimaye angerudiana na mzazi huyo mwenzake licha ya kutangaza kuwa amemalizana naye mwezi uliopita kufuatia drama iliyotokea  Dubai.

"Utarudi tuu 🤣😂🤣 utajirudisha mwenyewe!" @muthonipul alimwambia.

Karen alimjibu, "nikirudi uniite kang’ethe!"

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja baada ya mama huyo wa watoto watatu kukatiza uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu na Samidoh.

Karen alitangaza mwisho wa uhusiano wake na baba huyo wa watoto wake wawili katikati mwa Desemba kufuatia tukio la ugomvi uliowahusisha wao na mke wa Samidoh Edday Nderitu katika eneo moja la burudani jijini Dubai.

"Wanawake wakubwa na wajasiri watathibitisha kwamba mara nyingi kiungo chetu dhaifu ni wanaume tunaojihusisha nao. Ninaacha mtindo huo," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram mwezi jana.

Aliongeza "Nimefanya uamuzi wa kusitisha uhusiano wangu na baba wa watoto wangu na sasa ni mpenzi wa zamani."

Nyamu alibainisha kuwa hakuwa na majuto yoyote kufuatia  kile kilichotokea Dubai, na kuahidi kuwa tukio hilo lilikuwa la mwisho.

"Sitamani ningefanya mambo kwa njia tofauti," Nyamu alisema. "Najua nilipaswa kumpigia simu na kumaliza kimya kimya, lakini niliamua kuweka hadharani kama jinsi tu drama mambo tatanishi yamekuwa," aliongeza.

Hapo awali, Karen Nyamu, Samidoh na Edday Nderitu walikuwa wamehusika katika ugomvi ambao ulirekodiwa na video kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Wakenya watumizi wa mitandao ya kijamii walizungumza kuhusu drama hiyo kwa siku kadhaa huku wakitoa maoni tofauti kuhusu yaliyotokea.