“Nilistahimili” Esther Musila afunguka siku ya kwanza mbali na Guardian Angel ilivyokuwa

Musila alihofia kuwa siku yake ya kwanza kurudi kazini haingekuwa rahisi.

Muhtasari

•Musila alikuwa amedokeza kwamba haikuwa rahisi kwake kuwa mbali na mumewe kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu.

•Katika ripoti yake ya baada ya kazi hata hivyo, alisema kwamba aliweza kustahimili siku hiyo na alikuwa tayari kwa ya pili.

Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel, Esther Musila amebainisha kuwa aliweza kustahimili siku yake ya kwanza kazini baada ya miaka mitatu licha ya kueleza wasiwasi hapo awali.

Siku ya Jumatatu asubuhi, Musila alikuwa amedokeza kwamba haikuwa rahisi kwake kuwa mbali na mumewe kwa mara ya kwanza tangu janga la COVID-19 lilipovamia Kenya mapema mwaka wa 2020.

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alisema amekuwa akifanya kazi kutoka nyumbani kwa miaka mitatu ambayo imepita.

"Tangu COVID kuanza, tumekuwa pamoja kila siku. Leo ni siku ya kwanza tumetengana. Nitakumiss mpenzi lakini mtu lazima afanye kazi. Acha tuone jinsi itakavyokuwa. Muwe na siku njema," alisema Musila.

Musila alikuwa ametabiri kwamba siku yake ya kwanza kurudi kazini haingekuwa rahisi kwani alikuwa amezoea kuwa na Guardian Angel.

Katika ripoti yake ya baada ya kazi hata hivyo, alisema kwamba aliweza kustahimili siku hiyo na alikuwa tayari kwa ya pili.

"Ni siku nyingine mpya. Mungu ametupa zawadi na maisha, lazima tumshukuru. Ni siku ya pili. Kweli, nilistahimili jana," alisema kwenye video aliyochapisha Jumanne asubuhi na kuwatakia mashabiki wake siku njema.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 53 hufanya kazi katika ofisi za Umoja wa Kimataifa (UN) zilizo Gigiri,kaunti ya Nairobi.  Siku ya Jumatatu, alionyesha picha zake akiwa kazini na alionekana mwenye furaha.

Musila na Guardian Angel wamekuwa kwenye mahusiano kwa takriban miaka minne na walifunga pingu za maisha mapema mwaka jana.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Guardian Angel alibainisha kuwa amepata mafanikio mengi katika miaka minne ambayo wamekuwa pamoja.Alitaja uhusiano wake na Bi Musila kuwa muunganisho sahihi.

“Yamebadilisha maisha yangu, ukimsikiliza akiongea (Bi Musila) atasema jinsi mahusiano yetu yamebadilisha maisha yake,” alimwambia Willy Tuva.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 alidokeza kuwa athari chanya ya mahusiano yao ndilo jambo muhimu zaidi bila kujali maneno hasi kutoka ya wakosoaji .

Aidha, alifichua kwamba ameweza kukua katika nyanja nyingi za maisha tangu alipojuana na mwenzi huyo wake wa maisha.

“Nimeweza kuwa na ufanisi, nimeweza kukua, sio tu kimwili, lakini nimeweza kukua hata kiuchumi. Hata vitu kama hii ukulima yangu, na sifanyi ukulima kwa shamba ya watu, nafanya kwangu. Hiyo yote imeweza kufanyika kwa sababu ya muungano ambao niko nao na mke wangu," alisema Guardian Angel.

Mapema mwezi huu Musila alimhakikishia mwimbaji huyo wa nyimbo za injili kwamba hana majuto yoyote kwa kuamua kushiriki maisha naye huku akisema kuwa anaweza kufanya hivyo tena na tena.