Baada ya kujivinjari na Nyamu, Samidoh acheza kimahaba na mkewe hadharani (+video)

Wawili hao walicheza densi na kuburudisha wageni pamoja.

Muhtasari

•Edday alibainisha kwamba karamu hiyo iliyohudhuriwa na wanafamilia pamoja na marafiki wa karibu wa familia ilikuwa ya kusisimua.

•Wanandoa hao walionekana wakikumbatiana kwa mahaba huku wakinengua viuno kwa mitindo ya kimapenzi.

Samidoh, Edday Nderitu na Karen Nyamu
Image: HISANI

Wikendi, mwimbaji mashuhuri wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh na mke wake Bi Edday Nderitu waliandaa karamu kubwa nyumbani kwao kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya binti yao mdogo Neriah Wairimu.

Jumapili, Edday alibainisha kwamba karamu hiyo iliyohudhuriwa na wanafamilia pamoja na marafiki wa karibu wa familia ilikuwa ya kusisimua.

"Sherehe ya kupendeza ilikuwa, asante familia na marafiki kwa kujumuika nasi kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yangu ya kwanza, sherehe ilipamba moto, nguvu ilikuwa katika kiwango kingine," alisema kwenye Facebook.

Mama huyo wa watoto wawili aliendelea kumtakia baraka bintiye na kumhakikishia uwepo wake katika maisha yake.

"Umepamba maisha yetu kwa mwaka mzima sasa, ulikuja katika maisha yangu nilipokuhitaji sana, wewe ni baraka kwa familia yetu, ukue katika hekima na kimo. Mungu akulinde na mabaya yote," alimwandikia bintiye.

Mkewe Samidoh alionyesha picha kadhaa za karamu hiyo ya kukata na shoka ambayo ilifanyika nyumbani kwao. Pichani, yeye, mumewe na watoto wao watatu walionekana wenye furaha tele pamoja.

Video zilizochukuliwa wakati wa karama hiyo zinaonyesha wazazi wenza hao wawili wakicheza densi na kuburudisha wageni pamoja.

Huku wakidensi kwa wimbo wa hivi majuzi wa Samidoh na Prince Indah 'Bado Nakupenda', wanandoa hao walionekana wakikumbatiana kwa mahaba huku wakinengua viuno kwa mitindo ya kimapenzi.

Wikendi iliyopita, mwimbaji huyo wa Mugithi na mzazi mwenzake Karen Nyamu walikuwa miongoni mwa walioalikwa kwenye karamu ya kutoa shukrani ya waziri wa Biashara, Moses Kuria katika kaunti ya Kiambu.

Video za hafla hiyo ziliwaonyesha wapenzi hao wawili wakijivinjari pamoja wakati sherehe hiyo ikiendelea. Wawili hao ambao wana watoto wawili wadogo pamoja walionekana wenye furaha pamoja huku wakisherehekea.

Kwenye video moja, Bi Nyamu alitumia wimbo wa Jay Melody 'Sawa' kueleza nguvu ya mahaba yake na mwimbaji huyo wa Mugithi.

"Na penzi letu ni kama sunna

Na ulinzi kama suma

Hata akinuna

Bado unapendeza mchumba

Mkimuona ananichuna

Msinionee huruma

Cha mtu huliwa na mtu

Kutu yake chuma," aliimba pamoja na Melody.

Mama wa watoto watatu hata jina la Samidoh lilichorwa usoni mwake alipokuwa ameketi kando ya mzazi mwenzake.