"Penzi letu ni kama sunna" Karen Nyamu ajivinjari na Samidoh, achorwa jina lake usoni (+video)

Wawili hao ambao wana watoto wawili pamoja walionekana wenye furaha pamoja.

Muhtasari

•Seneta Karen Nyamu na mzazi mwenzake  Samidoh ni miongoni mwa walioalikwa kwenye karamu ya waziri Moses Kuria.

• Bi Nyamu alitumia wimbo wa Jay Melody 'Sawa' kueleza nguvu ya mahaba yake na mwimbaji huyo wa Mugithi.

Karen Nyamu na mzazi mwenzake Samidoh
Image: HISANI

Siku ya Jumapili, Waziri wa Biashara, Moses Kuria aliandaa karamu ya kutoa shukrani nyumbani kwake katika kaunti ya Kiambu ambapo aliwakaribisha viongozi kadhaa na watu wengine mashuhuri kutoka eneo la Mlima Kenya.

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh ni miongoni mwa walioalikwa kwenye karamu hiyo iliyofanyika baada ya ibada ya kutoa shukrani katika kanisa la Thika AIPCA Cathedral.

"Leo asubuhi niliungana na rafiki yangu wa muda mrefu, Waziri Moses Kuria kwa ibada yake ya shukrani katika Kanisa Kuu la AIPCA Thika," Samidoh alisema katika taarifa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii siku ya Jumapili.

Karen Nyamu kwa upande wake alitoa shukrani kwa waziri huyo kwa kuwakaribisha viongozi wa Mlima Kenya nyumbani kwake.

"Kikosi bila umoja hupigwa na fimbo moja. Asante Moses Kuria, waziri wa Biashara kwa kutukaribisha viongozi wa Mlima Kenya," alisema.

"Mashauriano yetu na maazimio yetu leo ​​yanafafanua mustakabali wetu kama jumuiya,

Mwanasiasa huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha kadhaa za karamu hiyo. Viongozi mashuhuri wa eneo la Mlima Kenya wakiwemo gavana Anne Waiguru, gavana wa Embu Cecily Mbarire, gavana wa Muranga Irungu Kang'ata, seneta wa Meru Kathuri Murungi na CAS Charles Njagua almaarufu Njagua walikuwepo.

Video moja inamuonyesha seneta Nyamu akijivinjari na mpenzi wake Samidoh wakati sherehe hiyo ikiendelea. Wawili hao ambao wana watoto wawili wadogo pamoja walionekana wenye furaha pamoja huku wakisherehekea.

Kwenye video hiyo, Bi Nyamu alitumia wimbo wa Jay Melody 'Sawa' kueleza nguvu ya mahaba yake na mwimbaji huyo wa Mugithi.

"Na penzi letu ni kama sunna

Na ulinzi kama suma

Hata akinuna

Bado unapendeza mchumba

Mkimuona ananichuna

Msinionee huruma

Cha mtu huliwa na mtu

Kutu yake chuma," aliimba pamoja na Melody.

Tazama video hapa:-

Mama wa watoto watatu hata jina la Samidoh lilichorwa usoni mwake alipokuwa ameketi kando ya mzazi mwenzake.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mkewe Samidoh, Edday Nderitu kudokeza kuhusu kuvunjika kwa ndoa yao.

Siku chache zilizopita, Bi Edday alizua tetesi za kuvunjika kwa ndoa yao ya takriban miaka kumi na mitano baada ya kushiriki katika challenge ya Tiktok inayovuma ya wimbo maarufu wa Harmonize  ‘Single Again.’ 

Mama huyo wa watoto watatu alichapisha video iliyomuonyesha akilala peke yake kwenye kochi huku akigugumia maneno ya wimbo huo.  Alionekana huru na mwenye furaha huku akiimba na staa huyo wa Bongo.