Mkewe Samidoh adokeza kuvunjika kwa ndoa yao baada ya kukataa kuwa mke mwenza wa Nyamu

Edday alionekana huru na mwenye furaha huku akidokeza yuko single.

Muhtasari

•Edday alichapisha video iliyomuonyesha akiwa amelala peke yake kwenye kochi huku akigugumia maneno ya wimbo wa Harmonize 'Single Again'

•Mashabiki wake waliotoa maoni walionekana kuusoma ujumbe huo kama tangazo kwamba hayuko tena na Samidoh.

Edday Nderitu, Karen Nyamu, Samidoh
Image: HISANI

Mke wa mwimbaji wa Mugithi Samidoh, Bi Edday Nderitu amezua tetesi za kuvunjika kwa ndoa yao ya miaka kumi na mitano baada ya kushiriki katika challenge ya Tiktok inayovuma ya wimbo wa Harmonize ‘Single Again.’ 

Siku ya Ijumaa, mama huyo wa watoto watatu alichapisha video fupi iliyomuonyesha akiwa amelala peke yake kwenye kochi huku akigugumia maneno ya wimbo huo mpya wa Konde Boy.

Kwenye video hiyo, Edday alionekana huru na mwenye furaha huku akiimba pamoja na staa huyo wa Bongo.

"Maybe this love is not for me,

I am single,

Do you know that I am single?

I am single again," aliimba.

Kumaanisha, {"Labda mapenzi haya sio yangu, niko single, Je, unajua kuwa niko single?, niko single tena."}

Baadhi ya mashabiki wake waliotoa maoni walionekana kusoma ujumbe huo kama tangazo kwamba hayuko tena na Samidoh.

Wengine wao walionekana kumshauri asiondoke kwa ndoa hiyo ambayo wamejenga kwa miaka mingi.

Ras Gal: Karibu kwenye klabu.

Annitah K: Soko ni chafu mami rudi kwako.

Single Queen: Kaa hapo usiende mahali wewe.

Rueben Maina: Bora sio mwenye vurugu ni kuhanyahanya tu kaa huko atachoka

Giar: Lakini kusema kweli watu single tuko na furaha kuliko walioolewa.

Mwezi uliopita, mama huyo wa watoto watatu alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Hii ilikuwa baada ya staa huyo wa Mugithi kuonekana na mzazi mwenzake, Karen Nyamu licha ya seneta huyo awali kutangaza uhusiano wao umefika mwisho. Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. 

Edday alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Licha ya yote, anasema, amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya mwanamuziki huyo.

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.

Edday alidai kuwa mzazi mwenza wa mumewe anamzidi umri kwa miaka kumi, sababu nyingine ya kufanya akatae awe mke mwenzake.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.

"Imekuwa miaka 15 kamili ya ndoa iliyojaa panda shuka, ilikuwa mwanzo mdogo ambapo kidogo ilikuwa ya kutosha kwetu, kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa maumivu,"