Stivo afunguka kuhusu kilichomvutia kwa mkewe, babake kutamani kumuona kabla ya kufariki

Rapa huyo alifichua amekuwa akichumbiana na Grace kwa takriban miaka minne iliyopita.

Muhtasari

•Stivo alidokeza kwamba alipima tabia za mke wake na za mpenzi wake wa zamani, Pritty Vishy na hatimaye kufanya uamuzi wake.

•Stivo aliweka wazi kwamba kwa sasa anaishi na mwenzi huyo wake wa maisha jijini Nairobi.

amemtambulisha mke wake Grace Atieno
Stivo Simple Boy amemtambulisha mke wake Grace Atieno
Image: HISANI

Mwimbaji Stephen Otieno Adera almaarufu Stivo Simple Boy amefichua kwamba tabia za mke wake Grace Atieno ndizo zilimvutia kwake.

Akizungumza kwenye mahojiano na Mungai Eve, rapa huyo alifichua amekuwa akichumbiana na Grace kwa takriban miaka minne iliyopita.

Stivo alidokeza kwamba alipima tabia za mke wake na za mpenzi wake wa zamani, Pritty Vishy na hatimaye kufanya uamuzi wake.

"Ukiwa na wasichana wawili unaangalia ni nani ako na utu, na ni nani ako wema na unyenyekevu. Kwangu mimi, unyenyekevu na kuvumilia kwake zilifanya nikavutiwa kwake," alisema msanii huyo kutoka mtaa wa Kibra.

Mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa hapo awali mkewe hakumuamini kabisa kwa kuwa aliamini dhana kuwa wasanii huwa na wapenzi wengi.

Alifichua kwamba Bi Grace aliamini mahusiano yao ni ya kweli baada ya kumtambulisha kwa wanafamilia wake.

"Hata kabla baba afariki, alikuwa anasema anataka kumuona. Lakini kwa bahati mbaya baba alifariki kabla ya kumuona," alisema.

Simple Boy alimtambulisha Grace Atieno kama mke wake halisi hadharani wakati wa hafla ya mazishi ya babake mnamo Februari 11.

"Bwana asifiwe. Kwa majina mimi ni Stephen Otieno. Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema mwimbaji huyo kabla ya kumpa kipaza sauti mke wake mrembo aliyesimama kando yake.

Baada ya kupokea kipaza sauti, Bi Atieno alimwomboleza baba mkwewe huku akionyesha wazi wazi ukaribu uliokuwepo kati yake na marehemu.

"Bwana asifiwe. Kwa majina ni Grace Atieno. Nimeoleka kwa Bwana Stephen Otieno. Naskia vibaya kumpoteza mtu mwenye alikuwa akinitoa kila wakati..." Grace alisema kabla ya kuzidiwa na hisia na kuangua kilio.

Kwenye mahojiano, Stivo aliweka wazi kwamba kwa sasa anaishi na mwenzi huyo wake wa maisha jijini Nairobi. Aliweka wazi kwamba yeye na Grace wanapendana sana na wanapanga kuendeleza mahusiano yao.

Hata hivyo, alibainisha kwamba bado hawajabarikiwa na mtoto pamoja.

Stivo aliachana na mtumbuizaji Pritty Vishy mapema mwaka jana, miezi michache tu baada ya uhusiano wao kujulikana hadharani.

Wawili hao hata hivyo ilidaiwa hawakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwani Stivo alidaiwa kutaka kusubiri ndoa kabla ya kushiriki tendo la ndoa na mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 21.