Rapa Octopizzo azungumzia bifu na Khaligraph Jones

Aliendelea kutoa pongezi kwa Papa Jones, akimtaka aendelee kutoa muziki mzuri.

Muhtasari

•Octo aliweka wazi kuwa bifu ina faida tu katika tasnia ya hip-hop wakati wahusika wanapata pesa kutoka kwayo.

Octopizzo na Khaligraph
Image: INSTAGRAM//

Rapa wa Kenya ambaye ni mshindi wa tuzo nyingi, Henry Ohanga, almaarufu Octopizzo, kwa mara nyingine tena amezungumza kuhusu bifu inayodaiwa kati yake na rapa mwenzake Brian Ouko Omollo almaarufu Khaligraph Jones.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Octo aliweka wazi kuwa bifu ina faida tu katika ulimwengu wa hip-hop wakati wahusika wanaohusika wanapata pesa kutoka kwayo.

Aliendelea kutoa pongezi kwa Papa Jones, akimtaka aendelee kutoa muziki mzuri.

“Huyo ni morio wangu na azidi kuweka bidii. Pigamawe,” Octopizzo alisema.

Rapa huyo alipoulizwa iwapo amesikiliza wimbo mpya wa Papa Jones uitwao Bang, alijibu; "Sijasikia wimbo lakini unaweza kunichezea ikiwa unayo. Kama ningeisikiliza, ningeweza kuizungumzia kwa urahisi kwa sababu ni mtu wangu.”