Alikiba amuonyesha upendo aliyekuwa mkewe, Amina Khalef licha ya ndoa kugonga ukuta

Alikiba hakuachwa nyuma katika kumsherehekea mzazi huyo mwenzake.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili alidokeza kwamba kadiri umri wake unavyosonga ndivyo anavyozidi kuwa jasiri.

•Alikiba alimtakia mama huyo wa watoto wake wawili kheri ya siku ya kuzaliwa na kumuombea baraka maishani.

Alikiba na aliyekuwa mke wake, Amina Khalef
Image: HISANI

Jumapili, Aprili 16, aliyekuwa mke wa msanii wa Bongo Ali Saleh Kiba almaarufu Alikiba, Amina Khalef aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Huku akijisherehekea, mama huyo wa watoto wawili alidokeza kwamba kadiri umri wake unavyosonga ndivyo anavyozidi kuwa jasiri.

"Mwaka mmoja zaidi, mwaka mmoja jasiri zaidi. Siku ya kuzaliwa yenye furaha kwangu," Bi Amina alijiandikia. 

Watu wake wengi wa karibu walitumia pia siku hiyo kumsherehekea mchambuzi huyo wa masuala ya fedha na kumtakia heri maishani.

Licha ya ndoa yao kuvunjika zaidi ya mwaka mmoja uliopita, Alikiba hakuachwa nyuma katika kumsherehekea mzazi huyo mwenzake.

Staa huyo wa Bongo alimtakia mama huyo wa watoto wake wawili kheri ya siku ya kuzaliwa na kumuombea baraka maishani.

"Happy birthday mama watoto. Allah akupe hitaji la moyo," Alikiba alimwandikia mkewe huyo wa zamani.

Aliambatanisha ujumbe huo na video yake akiwa na watoto wake wawili na Amina, Keyaan Kiba na Kamran Kiba.

Wakati akimjibu baba huyo wa wanawe, Bi Amina alimshukuru kwa kumtakia heri.

"Asante baba watoto," alijibu kwenye Instagram.

Talaka ya Alikiba na mzazi mwenzake Amina Khalef kutoka Kenya iligonga vichwa vya habari mapema mwaka jana.

Ombi la talaka liliwasilishwa mahakamani na Bi Amina mwezi Februari na kusikilizwa kwa miezi kadhaa kabla ya kuamuliwa.

Miezi kadhaa baadaye, mama huyo wa watoto wawili alitangaza kuwa yupo 'huru rasmi', ujumbe ambao ulieleweka kumaanisha kesi ilikuwa imekamilika.

Amina, ambaye sio maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii, alipakia picha ya ngome iliyo wazi na ndege akiruka.

Pia alifuta picha zote na AliKiba, zikiwemo zile za harusi yao ya kifahari iliyofanyika mnamo Aprili 2018.

Duru za kuaminika sasa zilisema AliKiba alijaribu kuokoa ndoa yake, ingawa mwishowe juhudi zake zikaambulia patupu.

“Tangu alipoomba talaka, Alikiba amesafiri kwenda Kenya mara nyingi akiwa hajitambui ili kujaribu kurekebisha mambo, lakini Amina alionekana kuwa ameamua,”  chanzo cha habari kilisema.

Kabla ya kudai talaka, inasemekana Amina alimpa mwimbaji huyo nafasi ya kurekebisha mambo, lakini hakufanya hivyo.

"Amina alikuwa ameamua kutulia na kulea familia na Ali," chanzo kilisema.

"Ilifika wakati alihisi kuwa alikuwa akimchukulia kawaida na hakuweza kuvumilia tena. Aliamua kuondoka."