Daddy Owen azungumzia kuachwa na mkewe kwa kukosa pesa, kutongozwa na wanawake

Owen alifichua kuwa wanawake walijaribu kumtongoza baada ya ndoa yake kuvunjika mwaka wa 2020.

Muhtasari

•Daddy Owen alidai kwamba hapo awali vyombo vya habari viliripoti kuwa aliachwa na aliyekuwa mke wake kwa sababu ya umasikini.

•Owen alifichua kwamba kuna wanawake wengi ambao humtumia jumbe tamu za mapenzi wakilenga kuchumbiana naye.

Image: INSTAGRAM// DADDY OWEN

Mwimbaji mkongwe wa nyimbo za Injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen amevikejeli vyombo vya habari kwa kutoa taarifa zinazokinzana kuhusu utajiri wake.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne kuhusu hosteli kubwa ya watoto wenye ulemavu ambayo ameijenga katika eneo la Kijabe, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 41 alidai kwamba hapo awali vyombo vya habari viliripoti kuwa aliachwa na aliyekuwa mke wake kwa sababu ya umasikini.

Huku akitupilia mbali tetesi hizo kwa njia isiyo ya moja kwa moja, Owen alibainisha kuwa kwa sasa vyombo vya habari vimejikita katika kuripoti kuhusu nyumba hiyo kubwa yenye thamani ya takriban milioni 37, jambo ambalo limefanya  jumbe za wanadada ambao wanammezea mate kumiminika kwenye simu yake.

"Eish! Watu ya media.. mara niliwachwa kwa sababu nimesota, alafu hii nayo imeleta shida pale kwa DM👆🏿. Sasa mnawachanganya maadui pamoja na wanaonimezea mate," alisema kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Kuhusu nyumba aliyojenga, mwimbaji huyo alisema, "Kutoa ni moyo usambe ni utajiri. Utukufu na heshima kwa Yesu Kristo."

Mwezi uliopita,  Owen alifichua kwamba kuna wanawake wengi ambao humtumia jumbe tamu za mapenzi wakilenga kuchumbiana naye huku wengine wakitumtumia picha za uchi wao wakikusudia kumtongoza.

"Tushazoea, ziko nyingi. Kwanza huwa nawablock mara moja," alisema kwenye mazungumzo na Shaffie Weru.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 41 alifichua kuwa wanawake walijaribu kumtongoza baada ya ndoa yake kuvunjika mwaka wa 2020. Alisema alipokea jumbe nyingi haswa kwenye mtandao wa Instagram.

Kwenye mahojiano na Plug TV mwaka jana, mwanamuziki huyo mahiri alidokeza kuwa tayari amemsamehe aliyekuwa mke wake, Farida Wambui kufuatia kutengana kwao takriban miaka mitatu iliyopita.

Owen hata hivyo aliweka wazi kuwa tangu wakati huo amesonga mbele na maisha yake na kudokeza kuwa si rahisi kwa wao kurudiana.

"Mimi ni mtu ambaye kitu ikifanyika nakusamehe lakini nasonga mbele. Kusonga nitasonga, lakini kusamehe nitasamehe," alisema.

Owen na mkewe wa kwanza Farida Wambui walitengana mwishoni mwa mwaka wa 2020 baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na masuala ya kutokuwepo kwa uaminifu katika ndoa.