"Kila siku niko single" Dadake Diamond akiri huku akifurahia kazi ya Harmonize

Esma amekuwa kwenye mahusiano kadhaa na hata ameolewa mara mbili.

Muhtasari

•Esma alijirekodi akiimba sehemu ya wimbo huo uliotolewa Jumanne wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Wapendanao.

•Esma alionekana kuufurahia sana wimbo huo na hata alisikika akiimba pia huku wimbo ukiendelea kucheza.

Diamond na dada yake Esma
Image: INSTAGRAM// ESMA KHAN

Video ya dada mkubwa wa staa wa bongofleva Diamond Platnumz, Esma Khan akifurahiya wimbo mpya wa Harmonize ‘Single Again’ inavuma kwenye mitandao ya kijamii.

Esma alikuwa kwenye gari na mwanamke mwingine alipojirekodi akiimba sehemu ya wimbo huo uliotolewa Jumanne wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Wapendanao.

“Masingle lady mmeona? Mimi kila siku niko single, sijui mwenzangu. Hadi siku ya Valentine's tupo single" alisikika akisema huku wimbo huo ukiendelea kucheza kwenye redio ya gari.

Mama huyo wa watoto watatu alionekana kuufurahia sana wimbo huo na hata alisikika akiimba pia huku wimbo ukiendelea kucheza.

Katika sehemu ya wimbo huo ambao umekuwa ukivuma kwenye majukwaa mbalimbali ya muziki, Harmonize anaimba, "I'm single. Do you know that I'm single? I'm single again! Who knows that I'm single? Ooh yes, I'm single. Ladies I'm single again!I 'm single. Who knows I'm single?"  ("Mimi niko single. Je, unajua niko single? Niko single tena! Nani anajua kuwa mimi niko single? Ooh kweli, niko single. Wanawake niko single tena. Niko single. Nani unajua mimi niko single?")

Esma amekuwa kwenye mahusiano kadhaa na hata ameolewa mara mbili Takriban miaka mitatu iliyopita, aligura ndoa yake na mfanyibiashara Yahya Msizwa miezi michache tu baada ya kufunga pingu za maisha.

Siku za hivi majuzi, Harmonize amekuwa akiweka wazi kwamba hayupo kwenye mahusiano yoyote baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake, muigizaji Frida Kajala Masanja mwishoni mwa mwaka uliopita.

Mapema mwezi huu, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alisema kwa sasa anajipatia muda usiojulikana wa mapumziko kabla ya kujitosa kwenye mahusiano mapya.

"Msijali, hivi karibuni nitapata mtu na mtamjua!!," alisema.

Staa huyo wa Bongopia alidokeza kwamba alipitia masaibu mengi mno wakati akiwa katika mahusiano yake ya awali.

Alionekana kuwakashifu wakosoaji na kuwataka wasite kumhukumu kwa kuwa hawana ufahamu wowote wa aliyopitia.

"Wasikuone na kidem tuu!! Hivi mnajua niliyo yapitia," aliandika.

Kajala alithibitisha kuvunjika kwa mahusiano yake na Harmonize mwezi Disemba baada ya kuchumbiana naye kwa takriban miezi saba.