"Ndio maana nilikuzaa, nitakuzaa tena" Samidoh amsherehekea marehemu mamake kwa njia maalum

"Popote ulipo, popote nitakapokwenda utabaki kuwa chanzo changu cha msukumo," alisema.

Muhtasari

•Samidoh alidokeza kuwa mzazi huyo wake marehemu Mirriam Wairimu ndiye msukumo wake mkuu maishani.

•Alidokeza kuwa ana mpango wa kuendeleza jina la mamake kwa kupata watoto zaidi wa kike atakaowaita Wairimu.

Samidoh na Marehemu Mirriam Wairimu
Image: INSTAGRAM/// SAMIDOH

Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh amemkumbuka marehemu mama yake ambaye alifariki miaka mingi iliyopita.

Katika chapisho lake la hivi punde, mwanamuziki huyo mahiri ambaye anashabikiwa sana hasa  katika eneo la Mlima Kenya alidokeza kuwa mzazi huyo wake marehemu Miriam Wairimu ndiye msukumo wake mkuu maishani.

"Popote ulipo, popote nitakapokwenda utabaki kuwa chanzo changu cha msukumo," alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha ya zamani ya marehemu mamake iliyopigwa wakati alipokuwa hai.

"Niko kwa sababu ulikuwa!" aliandika chini ya picha hiyo.

Alibainisha kuwa tayari amepata mabinti ambao amewapa jina la marehemu mama yake na kudokeza kuwa ana mpango wa kuendeleza jina hilo kwa kupata watoto zaidi wa kike ambao atawapa jina Wairimu.

'Ndio maana nilikuzaa na nitakuzaa tena!" alisema kwa lugha yake asili ya Kikuyu.

Mwimbaji huyo tayari ana mabinti wawili ambao wanaitwa Wairimu, mmoja alipata na mkewe Eddy Nderitu na mwingine na mwanasiasa Karen Nyamu.

Wanamitandao walitoa maoni kuhusu picha ya mzazi huyo wa Samidoh na baadhi walikuwa wepesi wa kugundua tabasamu sawa la marehemu na mwanawe. Bi Wairimu pia alikuwa na sifa zingine sawa na za mwanawe.

Marehemu Miriam Wairimu alikuwa mkulima mahiri na mwanamuziki kama mwanawe tu. Aliimba  nyimbo za injili.

Aliaga dunia wakati Samidoh akiwa bado katika shule ya upili. Baba yake pia alifariki wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017.

"Nilizaliwa katika familia ya watoto 6, sisi ni wavulana 6 na mimi ni wa tatu kuzaliwa. Mama alikuwa anaitwa Miriam Wairimu lakini alituacha. Na Mzee alikuwa anaitwa Michael Ndirangu. Alikuwa Afisa wa Polisi wa Utawala (AP). Alifanya kazi Nakuru na Molo na alikufa ile wakati wa mapigano,"  Samidoh alisema katika mahojiano ya awali.

Pia alifichua kwamba alikuwa akiimba pamoja na mamake kanisani na katika mikutano ya kidini. Alisema kuwa marehemu alichangia sana katika mafanikio yake kwenye tasnia ya muziki wa Kikuyu.