"Nikikukosa nitaumia sana!" Wema Sepetu akiri mahaba yake mazito kwa mpenziwe Whozu

Muigizaji huyo alimhakikishia mpenziwe kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kumuombea mema maishani.

Muhtasari

•Wema alimtambua mpenziwe kwa uhusika wake mkubwa katika maandalizi ya karamu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

•Wema alimuombea mpenziwe huyo maisha marefu na kudokeza kuwa angependa kushiriki maisha yake yote naye.

Wema Sepetu na Mpenzi wake Whozu
Image: INSTAGRAM

Kwa kweli muigizaji wa Bongo Wema Sepetu amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba na mpenziwe mpya Whozu.

Wema aliyaweka wazi mahusiano yake na mwimbaji huyo katika karamu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa iliyoandaliwa mapema wiki hii.

Wawili hao wamekuwa wakichumbiana kwa muda ila bado hawakuwa wamejitokeza hadharani kama wapenzi.

"Kwa muda mrefu nimekuwa sina raha. Nimekuwana huzuni, nimekuwa  nikilia lakini tangu nilipokutana na Chibaba wangu (Whozu) nimekuwa na raha na amekuwa akiweka tabasamu kwenye uso wangu," Wema alisema kwenye video ya moja kwa moja ya Instagram mnamo usiku wa kuamkia Jumatano.

Wapenzi hao walionekana wakijivinjari pamoja, wakikumbatiana, kudensi pamoja na hata kubusu mbele ya kamera kabla ya Wema kueleza jinsi alivyozama kwenye mahaba anayopewa na mwimbaji huyo.

Katika machapisho ya kuwashukuru waliofanikisha siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake, Wema alimtambua mpenziwe kwa uhusika wake mkubwa katika maandalizi ya karamu ya kusherehekea siku hiyo. Whozu ndiye aliyepanga na kugharamia karamu hiyo iliyohudhuriwa na marafiki kadhaa wa Wema.

"Asante kwa kila kitu mpenzi wangu. Unaweza kuona hiki ni kidogo bali hujui tu kina ukubwa gani umegusa moyo wangu," aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alisema anasubiri sana tarehe Machi 10 kufika ili aweze kumfanyia Whozu makubwa mnamo siku yake ya kuzaliwa kama njia ya kulipa ‘deni’ lake kubwa kwake. Pia alimhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kumuombea mema maishani.

“Yote tisa, nataka tu ujue unamaanisha ulimwengu kwangu. Na nitaendelea kukuombea kwa Mungu kila siku ya maisha yangu. Baraka zote zije kwako sababu unastahili kila jema katika maisha yako,” alisema.

Aliendelea kumuombea mpenzi huyo wake maisha marefu na kudokeza kuwa angependa kushiriki maisha yake yote naye.

“Umefanya msichana ajihisi amebarikiwa kwa mara nyingine maishani. Kupendwa raha sana. Roho yako nzuri ibarikiwe,”

Katika jibu lake kwa ujumbe huo, Whozu pia alimhakikishia mpenziwe huyo kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

“Unaweza ukajiona mwenye bahati lakini nataka ujue mimi ndiye mwenye Bahati kuwa chibaba wako. Nakupenda sana Chimama @wemasepetu,” alijibu.