"Nilikuwa na stress!" Diamond afarijika baada ya kurejeshewa cheni ya mamilioni ilioanguka jukwaani

Mkufu huo ulimgharimu Diamond takriban Tsh90M.

Muhtasari

•Mukufu huo ambao unameremeta kweli umeundwa kwa madini ya thamani yakiwemo dhahabu na Almasi.

•Aliyerejesha kipande hicho alidai kuwa alianzisha shughuli ya utafutaji punde baada ya kusikia kuwa Diamond alikipoteza akiwa jukwaani.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Diamond Platnumz alishindwa kuzuia furaha yake baada ya shabiki wake mmoja kumrejeshea kipande cha cheni yake ya dhahabu ambacho kilikuwa kimepotea.

Kipande maalum cha mkufu huo chenye maandishi 'SIMBA' kilikuwa kimeanguka wakati akitumbuiza jukwaani katika shoo yake ya Ureno.

Wakati akirejeshewa kipande hicho kinachokadiriwa kugharimu mamilioni ya pesa, Diamond alikiri kuwa alifadhaika sana baada ya kugundua kimepotea.

"Nilikuwa nimechizi, sikutaka kuonyesha, nilikuwa nimechizi. Nilikuwa nimepatwa na msongo wa mawazo kuhusu pambo langu hili," Diamond alisema baada ya kupokea kipande hicho.

Jamaa aliyerejesha kipande hicho alidai kuwa alianzisha shughuli ya utafutaji punde baada ya kusikia kuwa Diamond alikipoteza akiwa jukwaani.

Shabiki huyo ambaye alionekana mwenye furaha kubwa alichukua fursa hiyo kusherehekea matumbuizo ya ajabu ya Diamond na kumpongeza kwa kuunyanyua muziki wa Kiafrika kwa kiwango kikubwa zaidi.

"Nilienda kutafuta. Singeruhusu mtu yeyote aende na dola milioni hivo tu. Niko nawe ndugu yangu.  Hujawahi kuniangusha, haijawahi kutokea.Hatujawahi kuona chochote kama hichi. Ulitumbuiza vizuri, watazamaji walipenda.. endelea kufanya unachofanya," Shabiki huyo alimwambia Diamond.

Bosi huyo wa WCB alimshukuru shabiki huyo kwa kitendo hicho cha kushangaza na maneno ya kutia moyo aliyompa.

Agosti mwaka jana Diamond alionyesha mkufu huo wa thamani unaoripotiwa kumgharimu takriban millioni 90 za Tanzania (Ksh4.6M).

Cheni hiyo yenye umbo wa kichwa cha simba  ina maandishi 'SIMBA' kwa upande wa mbele na sura ya Diamond upande wa nyumba.

Mwaka jana cheni hiyo ilizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya mashabiki wakidai kuwa ni ishara kuwa ni ishara ushirikina.

Mukufu huo ambao unameremeta kweli umeundwa kwa madini ya thamani yakiwemo dhahabu na Almasi.