Nitaigharamia harusi ya Kajala na Harmonize- Irene Uwoya aahidi

Muhtasari

•Irene alitangaza kuwa yupo tayari kumvalisha muigizaji huyo mwenzake kutoka juu hadi chini bila kumdai chochote.

•Irene aliweka wazi kuwa hajawahi kutoa ushauri wowote kwa Kajala kuhusu mahusiano yake na Harmonize.

Harmonize na Kajala Masanja
Harmonize na Kajala Masanja
Image: HISANI

Muigizaji na mfanyibiashara Irene Uwoya ameahidi kugharamia mavazi ya Kajala mnamo siku ya harusi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika duka lake la nguo la Liz Payless, Irene alitangaza kuwa yupo tayari kumvalisha muigizaji huyo mwenzake kutoka juu hadi chini bila kumdai chochote.

Irene alibainisha kuwa atafurahi sana kumuona 'Drama Queen' huyo mwenzake akifunga pingu za maisha.

"Ni siku ambayo nitakuwa nimefurahi sana akiolewa. Mimi kwangu atapata ofa ya kila kitu. Kuanzia mwanzo wa kujiandaa mpaka wakati harusi itakapoisha, mimi nitasimama pale," Irene alisema.

Mfanyibiashara huyo alisema ukifika muda wa Harmonize na Kajala kufunga ndoa atawashauri wachukue nguo zote katika duka lake.

Irene hata hivyo aliweka wazi kuwa hajawahi kutoa ushauri wowote kwa Kajala kuhusu mahusiano yake na Harmonize.

"Mimi siwezi kuingilia mahusiano ya mtu. Mimi mwenyewe sipendi mwingine aingilie mahusiano yangu. Bora tu yupo na raha, niko nyuma yake," Alisema.

Harmonize na Kajala hatimaye walirudiana wiki kadhaa zilizopita baada ya kuwa wametengana kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Wawili hao walitengana Aprili mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa kipindi kifupi huku Harmonize akidaiwa kumtongoza bintiye Kajala, Paula.

Kabla ya kurudiana kwao alitumia mbinu nyingi za kuomba msamaha akiwa na lengo la kurejesha mahusiano yao.

Machi mwaka huu bosi huyo wa Konde Music Worlwide alitangaza utengano wake na Briana huku akidai kuwa nafsi yake ilimtaka Kajala tu.

"Kuhusu Briana, sina tatizo lolote naye. Ni mtu mzuri ila hatupo pamoja. Sababu ya kwanza, nilimwambia nimetengana na mtu bila kugombana naye na nampenda sana, sina uhakika kama nimemove on au lolote linaweza kutokea maana litakuwa tendo la kizalendo pia mimi kurudi nyumbani," Harmonize alisema.

Baada ya kutoa tangazo hilo Harmonize alijitosa kwenye safari ya kurejesha mahusiano yake na muigizaji huyo na kwa kweli juhudi zake zikazaa matunda hatimaye.

 Kajala sio mpenzi wa Harmonize tu ila sasa pia ndiye meneja wake na bosi wa mameneja wote wa Kondegang.