Pritty Vishy alia baada ya kutemwa na mpenziwe licha ya kuchorwa jina lake

Pritty Vishy amedokeza kwamba yupo sokoni kwa mara nyingine baada ya kutemwa na mpenzi wake.

Muhtasari

•Vishy alichapisha ujumbe wa huzuni akihutubia  mpenzi wake asiyejulikana ambaye alivunja moyo wake hivi majuzi licha ya kumpa mahaba mazito.

•Hivi majuzi, alifichua kwamba yuko kwenye uhusiano na mwanamume ambaye jina lake liliandikwa kwenye kidole chake.

Mwanablogu asherehekea siku yake ya kuzaliwa
Pritty Vish Mwanablogu asherehekea siku yake ya kuzaliwa
Image: Facebook

Muunda maudhui Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amedokeza kwamba yupo sokoni kwa mara nyingine baada ya kutemwa na mpenzi wake.

Siku ya Ijumaa, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 21 alichapisha ujumbe wa huzuni akihutubia  mpenzi wake asiyejulikana ambaye alivunja moyo wake hivi majuzi licha ya kumpa mahaba mazito.

Vishy alibainisha kuwa hata alichorwa tatoo ya mpenzi kutokana na upendo wake kwake lakini aliishia kumvunja moyo.

"Unampa mtu moyo wako na anacheza nao.. hadi unamchora tattoo lakini wapi," Pritty  Vishy alilalamika.

Mpenzi huyo wa zamani wa mwimbaji Stivo Simple Boy hata hivyo alidokeza kuwa yupo tayari kusonga mbele na maisha yake.

Hivi majuzi, alikuwa amefichua kwamba yuko kwenye uhusiano na mwanamume ambaye jina lake liliandikwa kwenye kidole chake.

"Sijui, lakini jina lake limechorwa kwenye kidole changu," alimjibu shabiki wake ambaye alihoji kuhusu hali yake ya mahusiano.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, alidokeza kuwa amepata mpenzi mpya ila akasema hayuko tayari kumuonesha  mitandaoni.

Hata hivyo, alidokeza kwamba mpenzi huyo wake  yupo kwenye mahusiano mengine ambayo alitaka kuyalinda.

“Sina uhakika wa kumpakia wakati wowote hivi karibuni kwa sababu ana mpenzi mwingine. Sitaki awachane na mchumba wake,” alisema.

Vishy alitengana na Simple Boy mapema mwaka jana, miezi michache tu baada ya mahusiano yao kujulikana hadharani.

Wawili hao hata hivyo ilidaiwa hawakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwani Stivo alidaiwa kutaka kusubiri ndoa kabla ya kushiriki tendo la ndoa na mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 21.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Stivo alidokeza kwamba alichumbiana na Pritty Vishy wakati bado akiwa na mke wake, Grace Atieno. Alisema alipima tabia za wawili hao kabla ya kuamua mke wa kuwa naye. 

"Ukiwa na wasichana wawili unaangalia ni nani ako na utu, na ni nani ako wema na unyenyekevu. Kwangu mimi, unyenyekevu na kuvumilia kwake zilifanya nikavutiwa kwake," alisema msanii huyo kutoka mtaa wa Kibera.

Simple Boy alimtambulisha Grace kama mke wake halisi hadharani wakati wa hafla ya mazishi ya babake mnamo Februari 11.

"Bwana asifiwe. Kwa majina mimi ni Stephen Otieno. Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema mwimbaji huyo kabla ya kumpa kipaza sauti mke wake mrembo aliyesimama kando yake.