"Tatizo la Omosh ni nini?" Akothee aomba majibu baada ya muigizaji huyo kutaka usaidizi tena

Omosh alikiri kuwa hayuko sawa na kudokeza kuwa haishi tena na familia yake.

Muhtasari

•Siku kadhaa zilizopita Omosh alidokeza kuwa hayuko sawa na kufichua amepoteza takriban kila kitu ikiwa ni pamoja na familia yake.

•Akothee ametaka Omosh kufunga kuhusu matatizo yanayomsababishia msongo wa mawazo ili aweze kusaidika.

Omosh Kizangila, Akothee
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji tajiri Akothee ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya aliyekuwa mwigizaji wa Tahidi High Joseph Kinuthia almaarufu Omosh.

Siku kadhaa zilizopita Omosh alidokeza kuwa hayuko sawa na kufichua amepoteza takriban kila kitu ikiwa ni pamoja na familia yake.

Akothee sasa amemfariji muigizaji huyo na kupendekeza kutafutwa kwa suluhu la kudumu la matatizo mengi ambayo yamekuwa yakimkumba.

"Omosh! Pole kwa yote unayopitia, hauko peke yako ndugu yangu. 80% ya Wakenya wanapitia matatizo mabaya zaidi ambayo hata hawajui ikiwa pamoja na matatizo ya kiakili," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa Wakenya wengi wanakumbwa na matatizo ya kifedha ambayo yamewasababishia msongo wa mawazo.

Aliendelea kutaka Omosh kufunga kuhusu matatizo yanayomsababishia msongo wa mawazo ili aweze kusaidika.

"Omosh ni nini kinakutatiza ili tuanze kukishughulikia? Unaona vipi tunaweza kukusaidia?" alimuuliza muigizaji huyo.

Aliendelea, "Ni wewe utuambie hii stori yako tumalize tuendelee na maisha ingine. Jamani, tatizo la Omosh ni nini?"

Katika mahijiano na Mpasho wiki jana, Omosh alikiri kuwa hayuko sawa.

"Ninapitia mengi tu, sijui ni msongo wa mawazo au nini kinatokea katika maisha yangu,"

Muigizaji huyo pia alidokeza kuwa haishi tena na familia yake.

"Nimepoteza kila kitu katika maisha yangu, mke wangu, na kila kitu kimeenda,"

Omosh alifunguka kwa mara ya kwanza kuhusu matatizo yake ya kifedha mwaka jana ambapo alijitokeza kuomba msaada.

Wakenya wa tabaka mbalimbali walijitolea kumsaidia kwa michango ya kila aina ikiwemo pamoja na kumjengea nyumba.

Miezi michache baadae hata hivyo muigizaji huyo alijitokeza tena kuomba msaada huku akidai kuwa amefilisika. Wakati huo alidai kuwa baadhi ya watu ambao waliahidi kumsaidia hawakutimiza ahadi zao.

Masaibu ya muigizaji huyo yamekuwa yakihusishwa na uraibu wa pombe ambao aliwahi kukiri amepambana nao kwa miaka mingi.