Zari kusherehekea Krismasi na Diamond licha ya Zuchu 'kumrithi'

Baadhi wamedai kuwa ana mpango wa kuvuruga mahusiano ya Diamond na Zuchu.

Muhtasari

•Kumekuwa na tetesi kuwa mwanasoshalaiti huyo alipanga ziara hiyo baada ya Diamond na Zuchu kutangaza mahusiano yao.

•Zari pia yupo kwenye mahusiano na kijana wa miaka 30, Shakib Cham.

Diamond Platnumz, Prince Nillan, Tiffah Dangote na Zari Hassan
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mpenzi wa zamani wa Diamond Platnumz, Zari Hassan atakuwa nchini Tanzania katika kipindi cha  Krismasi mwezi ujao.

Mwanasoshalaiti huyo mzaliwa wa Uganda alishiriki mazungumzo ya simu na Mama Dangote ambapo alimthibitishia kuhusu ziara hiyo ya Desemba. Alimwambia mzazi huyo wa Diamond kwamba atawapeleka wajukuu wake Tiffah Dangote na Prince Nillan ili waweze kufurahia muda na wanafamilia wengine.

Katika mazungumzo hayo, Zari ambaye kwa sasa anaishi na familia yake Afrika Kusini alidokeza kuwa mpango wa kusherehekea sikukuu ya Krismasi nchini Tanzania ni uamuzi ambao alifanya pamoja na Diamond.

"Baba yao amesema wanakuja Krismasi. Bado tuko shule," Zari alimwambia Mama Dangote katika mazungumzo.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Zari Hassan na watoto wake kutembelea familia ya kina Diamond katika miaka ya hivi majuzi. Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 42 bado huwa anatembea nyumbani kwa mzazi huyo mwenzake licha ya wao kutengana takriban miaka minne iliyopita.

Mara nyingi anapozuru Tanzania, mama huyo wa watoto watano huwa ameandamana na watoto wake na Diamond, Tiffah na Nillan. Yeye na watoto hao wake wadogo wamehifadhi uhusiano mzuri na familia ya staa huyo wa Bongo licha ya tofauti zilizotokea hadi kuvunja mahusianoi yao ya muda mrefu.

Hata hivyo, kumekuwa na tetesi kuwa mwanasoshalaiti huyo alipanga ziara hiyo baada ya Diamond na Zuchu kutangaza mahusiano yao. Baadhi wamedai kuwa anapanga kuvuruga mahusiano ya wawili hao.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Mama Dangote kuthibitisha kuwa mwanawe Diamond yupo kwenye mahusiano na Zuchu. Mapema mwezi huu, alipakia video ya msanii huyo kutoka Zanzibar na kumsherehekea huku akimtakia heri za siku ya kuzaliwa.

"Nakutakia maisha marefu yenye Baraka... Ma mkwe Zuhura Othman Suod @officialzuchu 💕💕💕," aliandika.

Zuchu alimjibu Mama Dangote na kumshukuru kwa kumtakia mema.

"❤️❤️❤️ asante mamaangu 😍😍," Zuchu alisema.

Vilevile, hivi majuzi Diamond alichapisha video ilionyesha wakionyesha mahaba tele na Zuchu na kubusu.

Zari pia yupo kwenye mahusiano na kijana wa miaka 30, Shakib Cham.