Grand P ajigamba kuhusu mahaba mazito anayopewa na mpenziwe mpya baada ya kumtema Yao

Mwimbaji huyo alisifia mapenzi matamu ambayo amekuwa akipewa na Mchina huyo.

Muhtasari

•Grand P alimtambulisha mpenzi wake mpya , Yubai Zhang mwezi uliopita na wamekuwa wakijivanjari pamoja na kuonyesha muungano wao mzuri.

•Wawili hao walianza kuchumbiana miezi kadhaa baada ya mahusiano ya Grand P na mwanasoshalaiti Eudoxie Yao kugonga mwamba.

Eudoxie Yao, Grand P na Yubai Zhang
Image: HISANI

Ni wazi kuwa mwimbaji mbilikimo kutoka Guinea Moussa Sandiana Kaba almaarufu Grand P kwa sasa anaogelea kwenye mahaba mazito.

Mwanamuziki huyo mwenye maumbile ya kipekee alimtambulisha mpenzi wake mpya mwenye asili ya Asia, Yubai Zhang mwezi uliopita na wawili hao wamekuwa wakijivanjari pamoja na kuonyesha muungano wao mzuri.

Siku ya Jumatatu, Grand P alijigamba kuhusu mapenzi matamu ambayo amekuwa akipewa na kipusa huyo.

"I am a spoiled baby by Yubai Zhang❤," alisema kwenye picha yake na Zhang aliypchapisha kwenye Instagram.

Kumaanisha, "Mimi ni mtoto aliyeharibiwa."

Mwimbaji huyo maarufu na mpenziwe mpya wamekuwa wakisafiri katika nchi tofauti pamoja na kujivinjari pamoja katika sehemu mbalimbali. Wawili hao hawajaona haya kukiri mapenzi yao mazito licha ya tofauti zao.

"Niko pamoja na mpenzi wangu Grand P, safari yangu nyingine inakuja hivi karibuni," Bi Zhang alisema siku kadhaa zilizopita kwenye video iliyomuonyesha akifurahia muda na msanii huyo anayeaminika kuwa mbwenyenye.

Wiki iliyopita, Grand P alithibitisha mapenzi yake na mrembo huyo  na kuweka wazi hakuna nafasi ya watu wenye wivu maishani mwao.

"Yubai Zhang wangu, hakuna nafasi kwa watu wenye wivu," alisema chini ya picha zake na Zhang alizochapisha Facebook.

Wapenzi hao walianza kuchumbiana miezi kadhaa baada ya mahusiano ya Grand P na mwanasoshalaiti wa Ivory Coast mwenye umbo la kustaajabisha kweli, Eudoxie Yao  kufika kikomo mapema mwaka jana kwa njia isiyoeleweka baada ya wawili hao kuchumbiana kwa takriban miaka mitatu.

Mwezi Mei, mwaka jana, mwanamuziki huyo alikuwa amedhihirisha mahaba yake makubwa kwa Eudozie Yao kwa kuchorwa tattoo ya jina lake mkononi. Alichorwa "Love Eudoxie" kwenye kifundo cha mkono wake wa kushoto.

Mwanasoshalaiti huyo alisherehekea kitendo hicho  na kubainisha kuwa mapenzi ambayo mumewe anampa ni matamu mno.

"Nani ana mapenzi matamu kama haya? Mpenzi wangu Grand P," Eudoxie alisema kupitia Facebook.

Wawili hao pia walikuwa wamedokeza ndoa huku Grand P akimvisha mlimbwende huyo pete ya uchumba mapema mwaka jana.