Ida Odinga alicheka nilipomwambia nina mimba ya mtoto wa 6- Akothee afunguka

Alifichua alifichua kwamba alipopoteza ujauzito, alizungumza na Ida na hilo lilimfanya ajisikie vizuri.

Muhtasari

•Akothee alifichua Ida amekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujua kuhusu maendeleo mapya katika maisha mwake.

•Akothee alisema kwamba Ida alikubali kuhudhuria harusi yake mnamo Aprili 10 mara tu alipomwalika.

mnamo Aprili 10, 2023.
Ida Odinga na Akothee mnamo Aprili 10, 2023.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Akothee amedokeza kuhusu uhusiano wake wa karibu na mke wa kiongozi wa muungano wa Azimio-One Kenya Raila Odinga, Ida Odinga.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa kila wakati Bi. Ida amekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kujua kuhusu maendeleo mapya katika maisha mwake.

"Nilipokutana na Omosh, nilimweleza (Ida) habari hizo, Omosh aliponichumbia na tukapanga tarehe ya harusi yangu, alikuwa wa kwanza kupata habari hizo kabla ya mtu mwingine yeyote. Nilipopata ujauzito katika wiki 6, nilimpigia simu na kumwambia. Mama tuna mimba 🙊," Akothee alisimulia.

Mwanamuziki huyo alisema baada ya Ida kusikia ana ujauzito wa ambaye angekuwa mtoto wake wa sita, alicheka kwanza kisha akampongeza. Pia alifichua kuwa mke huyo wa Raila alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujua kwamba alikuwa amepoteza ujauzito wake ambapo baadaye walizungumza kuhusu suala hilo.

"Ananielewa kama vile mama angemuelewa binti yake, anajua natamani mapenzi kwa hiyo mlango wake uko wazi kwa ajili yangu 24/7, Tulipopoteza ujauzito, katika wiki 10, alipiga simu na tukazungumza mengi, nilijisikia vizuri 🙏," alisema.

Pia alifichua kuwa alimtambulisha mume wake Denis Shweizer almaarufu Omosh kwa Ida ili kupata kibali chake kabla ya harusi yao.

"Aliuliza mengi kuhusu Omosh ikiwa ni pamoja na historia yake na familia. Nilimhakikishia kuwa nimekutana na familia yake hata hivyo wao sio watu wa mitandao ya kijamii. Wanaishi maisha ya faragha sana, na kilichokuwa cha kutisha kwa mama Omosh ni kumtambulisha Omosh kwa mashabiki wangu," alisema.

Mama huyo wa watoto watano alisema kwamba Ida alikubali kuhudhuria harusi yake mnamo Aprili 10 mara tu alipomwalika.

"Nakupenda, mama Ida Odinga. Ubarikiwe kwa kuinua roho yangu kila wakati," alimwambia.

Bi Ida Odinga alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri ambao walihudhuria harusi ya Akothee na Shweizer siku ya Jumatatu.

Wengine ni pamoja na:-

  • Millie Odhiambo (Mbunge Suba Kaskazini)
  • Aisha Jumwa (Waziri wa Jinsia & Uutumishi wa umma)
  • Karen Nyamu (Seneta wa Kuteuliwa)
  • Phelix ‘Jalango’ Odiwour (Mbunge Lang’ata)
  • Ruth Odinga (Mwakilishi Wanawake Kisumu)
  • Dorothy Ngong’o (Mkewe gavana Anyang’ Nyong’o)
  • Agnes Ayacko (Mkewe gavana Ochilo Ayacko)
  • Suleiman Shabal (Aliyekuwa mgombea ugavana Mombasa)
  • David Osiany (CAS Biashara)