Inauma! Mwili wa 2Pac wa Ghana wasimamishwa kando ya jeneza kupewa heshima ya mwisho (+picha)

Alizikwa kwenye jeneza la rangi ya dhahabu lililokuwa na lebo ya Tiktok.

Muhtasari

•Mamia ya waombolezaji wakiwemo wanafamilia, marafiki, wasanii na watu wengine mashuhuri walihudhuria hafla hiyo iliyojaa hisia.

•Kabla ya kuzikwa, mwili wa Ahoufe ulitolewa nje ya jeneza ili kuwaruhusu waombolezaji kumpa heshima za mwisho.

Marehemu Ahoufe Abrantie

2pac Shakur wa Ghana,  Ahoufe Abrantie hatimaye alizikwa mwishoni mwa mwezi jana.

Mtumbuizaji huyo wa Tiktok mwenye maumbile ya kipekee ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kote duniani kupitia video zake za kusisimua alizikwa nyumbani kwao katika eneo la Kumasi, Ghana mnamo Aprili 29.

Mamia ya waombolezaji wakiwemo wanafamilia, marafiki, wasanii na watu wengine mashuhuri walihudhuria hafla hiyo iliyojaa hisia. Alizikwa kwenye jeneza la rangi ya dhahabu lililokuwa na lebo ya Tiktok.

Kabla ya kuzikwa, mwili wa Ahoufe ulitolewa nje ya jeneza ili kuwaruhusu waombolezaji kumpa heshima za mwisho.

Video za mazishi hayo ambazo zilifikia Radio Jambo ziliwaonyesha waombolezaji wakifanya matambiko mbalimbali kwenye mwili wa mtumbuizaji huyo huku wengine wao wakiangua kilio kikubwa baada ya kuutazama mwili. Mwili wa marehemu Ahoufe uliokuwa umevalishwa shati ya bluu, bandana kichwani na mnyororo shingoni ulitulia pembeni ya jeneza huku waombolezaji wakitoa heshima za mwisho.

Staa huyo wa TikTok aliaga dunia mnamo Machi 30 katika nyumba yake jijini Kumasi, Ghana. Kifo cha Ahuofe ambaye alijulikana sana kwa kuvaa na kuzungumza kama ‘jambazi’ kiliwashangaza wengi ambao walimuomboleza kwa hisia.

Video zake zilihusu kuiga haiba ya marehemu rapa wa Marekani, Tupac Amaru Shakur.

Huku akimuomboleza, mama yake alisema, "Alilazwa hospitalini kwa siku mbili kabla ya kifo chake. Uvumi kwamba alikuwa akitumia dawa za kulevya ni uongo. Nilitokwa na machozi daktari alipothibitisha kifo chake. Nawashukuru mashabiki wake kwa upendo. Mungu atusaidie."

Mamake Ahuofe ambaye anajulikana sana kama Mama gee alisema ilimletea furaha kuona jinsi mwanawe alivyosababisha furaha kubwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Hakuwa na tatizo la kiafya," alisema.