Eric Omondi aendeleza ugomvi na Bien kwa ngoma

Muhtasari

• Ugomvi kati ya mchekeshaji Eric Omondi na mwanzamuziki kutoka kundi la Sauti Sol, Bien Baraza uko mbali sana na kufikia kikomo

• Katika wimbo huo maarufu kwa wakenya kama ‘diss track’ Omondi anatumia suala zima la upara wa Bien Aime Baraza kama kigezo cha kumpasha.

Bien Baraza na Eric Omondi
Image: Facebook

Ugomvi kati ya mchekeshaji Eric Omondi na mwanzamuziki kutoka kundi la Sauti Sol, Bien Baraza uko mbali sana na kufikia kikomo, yaani kama vipi ndio mwanzo mkoko unaalika maua.

Hii ni baada ya mchekeshaji Omondi kufanya ‘cover’ ya wimbo wa Bien Baraza wa Mbwe Mbwe aliomshirikisha Aaron Rimbui ambapo anamkashfu Barasa kutokana na upara wake.

Katika wimbo huo maarufu kwa wakenya kama ‘diss track’ Omondi anatumia suala zima la upara wa Bien Aime Baraza kama kigezo cha kumpasha.

Watu wengi wamefurahia ufundi wa Omondi katika wimbo huo kutokana na jinsi alivyoyaingiza maneno yake kwenye mindundo ya muziki wa Barasa kwa ufasaha usio na kifani.

Kutokana na ucheshi wake katika video hiyo ambayo Omondi ameipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram Februari 7, wengi wamesema wawili hao hawana uhasama ila ni mbwe mbwe tu za kuleta uhai katika tasnia ya muziki nchini Kenya.

Ugomvi wa wawili hawa umedumu Zaidi ya miezi miwili baada yao kuburuzana mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana katika hafla ya msanii kutoka Jamaica, Konsens ambapo baadaye Barazac alimtuhumu Omondi kwa kumuibia vitu vya kibinafsi kama ufunguo wa gari, simu na kitambulisho.